RIADHA

Kenyatta atia saini sheria ya kukataza dawa za kusisimua misuli

Rais Uhuru Kenyatta akisaini mswada huo kuwa sheria
Rais Uhuru Kenyatta akisaini mswada huo kuwa sheria State House Nairobi

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ametia saini mswada wa kukabiliana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini kwa wanamichezo kuwa sheria.

Matangazo ya kibiashara

Sheria hii inamaanisha kuwa, Kenya sasa itakuwa inashirikiana kikamilifu na Shirika la Kimataifa linalopambana na dawa hizo WADA kupiga vita janga hili.

Kenya ililazimika kuwa na sheria hii baada ya WADA kuiorodhesha kama mojawapo ya nchi ambazo zimekataa kutoa ushirikiano na hivyo, baada ya kuwepo kwa madai kuwa wanariadha wake wanatumia dawa hizo.

Mwezi uliopita, ujumbe wa serikali ya Kenya ulikwenda katika makao makuu ya WADA mjini Montreal nchini Canada kujadiliana kwa kina kuhusu sheria hii mpya baada ya sheria ya awali kukataliwa na Shirika hilo.

Rais Uhuru  Kenyatta (Kulia) akisalimiana na viongozi wa Shirikisho la riadha AK Juni 23 2016, Ikulu Nairobi
Rais Uhuru Kenyatta (Kulia) akisalimiana na viongozi wa Shirikisho la riadha AK Juni 23 2016, Ikulu Nairobi State House Nairobi

Kuwepo kwa sheria hii kunamaanisha kuwa wanariadha na wanamichezo wengine nchini humo watakuwa huru kushiriki kikamilifu katika mashindano ya Olimpiki mwezi Agosti mwaka huu nchini Brazil.

Wanariadha wa Kenya walianza kutiliwa shaka baada ya kuongoza dunia wakati wa mashindano ya Olimpiki jijini London nchini Uingereza mwaka 2012.

Rais Kenyatta amesema, nchi yake imekuwa ikiunga mkono kuwepo kwa ukweli katika michezo na itaendelea kufanya hivyo.