EURO 2016

Sweden yatupwa nje, Ureno yaponea chupuchupu

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic REUTERS/Stephane Mahe

Michuano ya kombe la mataifa ya Ulaya 2016, sasa imefikia mahali pazuri, baada ya kutamatika kwa mechi za mwisho za hatua ya makundi, ambapo mechi za kundi, E na F zilichezwa. 

Matangazo ya kibiashara

Mechi ambayo ilivuta hisia za watu wengi ni ile ya mchezo wa kundi F, ambapo ulizikutanisha timu ya taifa ya Ureno dhidi ya Hungary, mchezo ambao ulikuwa ni muhimu wa Ureno kuibuka na ushindi ili ikate tiketi ya kuingia hatua ya 16 bora.

Mechi hiyo hata hivyo ilitamatika kwa timu zote kutoshana nguvu kwa kufungana mabao 3-3, mechi ambayo ilishuhudia timu zote zikifanya mashambulizi ya piga nikupige kwa muda wote wa dakika 90.

Katika mchezo huo mchezaji wa Ureno na nahodha wa timu hiyo, Christian Ronaldo, hatimaye alimaliza ukame wa kutofunga goli toka kuanza kwa michuano ya mwaka huu, ambapo alipachika mabao 2.

Magoli ya Hungary, yalifungwa na wachezaji, Zoltan Gera na Balazs Dzsudzsák aliyefunga magoli mawili, huku yale ya Ureno, yakifungwa na wachezahi Luis Nani na mengine mawili yakifungwa na Christian Ronaldo.

Licha ya kuambulia sare na kumaliza kwenye nafasi ya tatu kwenye kundi lake, timu ya taifa ya Ureno imekata tiketi ya kucheza hatua ya mtoano.

Kwenye mchezo mwingine, timu ya taifa ya Iceland ilifanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao 2-1 dhidik ya Austria, mchezo ambao toka mwanzo, Iceland walionekana kuwa na nia ya kuibuka na ushindi jambo ambalo hadi dakika tisini zinamalizika waliibuka washindi.

Katika mechi za kundi E, timu ya taifa ya Italia ilikuwa na kibarua dhidi ya Jamhuri ya Ireland katika mchezo ambao Italia walikuwa wakicheza huku wakijua tayari wameshakata tiketi hatua ya mtoano, na badala yake ulikuwa ni mchezo muhimu kwa timu ya taifa ya Ireland.

Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila ya timu yoyote kupata bao, kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo kilishuhudia timu zote mbili zikifanya kila namna kuhakikisha zinatapa ushindi, mikakati ambayo ilifanya kazi kwa timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mechi nyingine ilikuwa nik kati ya timu ya taifa ya Sweden iliyokuwa na kibarua dhidi ya Ubelgiji, kwenye mchezo ambao ulishuhudia, Sweden ikiaga mashindano ya mwaka huu kwenye hatua ya makundi, kwa kukubali kichapo cha goli 1-0.

Bao pekee la Ubelgiji lilifungwa katika dakika ya 86 ya mchezo na mchezaji, Radja Nainggolan aliyepokea pasi kutoka kwa nahodha wa timu hiyo, Eden Hazard.

Matokeo haya sasa kutoka kundi F, timu zilizofuzu hatua ya mtoano ni, Hungary ambao walikuwa vinara, Iceland waliomaliza kwenye nafasi ya pili, na Ureno waliomaliza kwenye nafasi ya tatu bora.

Katika kundi E, timu zilizofuzu ni pamoja na Italia ambao walimaliza kama vinara wa kundi lake, Ubelgiji waliomaliza nafasi ya pili wakilingana alama na Italia ila wakitofautiana magoli ya kufunga na kufungwa, huku Jamhuri ya Ireland nayo ikipata nafasi kwa kumaliza kwenye nafasi ya tatu bora.