OLIMPIKI RIO

Wanamichezo wa Urusi, Kazakhstan na Belarus, matatani tena

Mmoja wa wanamichezo wanao nyanyua vitu vizito.
Mmoja wa wanamichezo wanao nyanyua vitu vizito. REUTERS

Timu za wanyanyua vitu vizito kutoka mataifa ya Urusi, Kazakhstan na Belarus, huenda wakazuiwa kushiriki michezo ya Olimpiki ya mjini Rio, Brazil, kwa tuhuma za wachezaji wake kukwepa vipimo vya kubaini ikiwa walitumia dawa za kusisimua misuli au la. 

Matangazo ya kibiashara

Shirikisho la kimataifa la mchezo wa kunyanyua vitu vizito, IWF, limesema kuwa zuio hilo linahusu sampuli zilizorudiwa kupimwa upya wakati wa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 na 2012.

IWF inasema kuwa adhabu hii ya kufungiwa kwa mwaka mmoja, itahitaji kwanza kuthibitishwa na kamati ya dunia ya Olimpiki, IOC.

Kwenye taarifa yake, shirikisho la kimataifa la mchezo wakunyanyua vitu vizito, inasema kuwa "ni wachezaji walio wasafi tu ndio watakaoruhusiwa kushiriki."

Hata hivyo shirikisho la IWF halijaweka wazi majina ya wanamichezo ambao sampuli zao zilirejelewa kupimwa na sasa watakumbana na adhabu hiyo.

IWF imetangaza kuwa itawachukulia hatua wanamichezo kutoka mashirikisho ambayo yamethibitika kukiuka kwa zaidi ya mara tatu sheria na kanuni za kuwapima wanamichezo wao kubaini ikiwa walitumia dawa za kusisimua misuli au la na sampuli zao zilichukuliwa kutoka kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008 na London mwaka 2012.

Taarifa hii imetolewa kufuatia uthibitisho uliotolewa juma lililopita, kuwa wanamichezo wanne wa kunyanyua vitu vizito walioshiriki Michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012 kutoka nchini Kazakhstan, akiwemo bingwa mara nne wa mchezo hio, IIya IIyin, ambaye vipimo vyake vimeonesha kuwa chanya.

Wanamichezo wengine 6 walioshiriki michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012, pia vipimo vyao vimeonesha kuwa chanya baada ya mamia ya sampuli za wanamichezo walioshiriki michezo hiyo kupimwa upya.

Wiki iliyopita Shirikisho la kimataifa la riadha IAAF, liliamua kutoondoa makataa yake kwa nchi ya Urusi, adhabu iliyotolewa mwaka jana, baada ya nchi hiyo kubainika kuwa ilisaidia wanariadha wake kukwepa vipimo.