CAF

CAF yaishushia rungu klabu ya Setif ya Algeria

Wachezaji wa klabu ya E.S Setif ya Algeria wakiwa hawaamini kinachotokea uwanjani baada ya mashabiki wao kufanya vurugu kwenye mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, mchezo wa klabu bingwa Afrika, Juni 18, 2016
Wachezaji wa klabu ya E.S Setif ya Algeria wakiwa hawaamini kinachotokea uwanjani baada ya mashabiki wao kufanya vurugu kwenye mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, mchezo wa klabu bingwa Afrika, Juni 18, 2016 DR

Timu ya Entente Setif ya Algeria imeondolewa kushiriki michuano ya kombe la klabu bingwa barani Afrika inayosimamiwa na CAF, baada ya vurugu zilizojitokeza kwenye mchezo wake dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Mchezo huo uliochezwa Juni 18, haukumalizika kwa dakika 90, baada ya mwamuzi wa mchezo huo, kuamua kuumaliza kabla ya muda wakati Mamelodi ikiwa inaongoza kwa mabao 2-0.

Mwamuzi wa mchezo huo alilazimika kuusimamisha kwa muda mchezo kutokana na vurugu zilizojitokeza kwenye jukwaa la mashabiki wa Etente Setif, ambao walianza kurusha mawe na fataki uwanjani, hatua iliyosababisha mwamuzi kuamua kumaliza mchezo kabla ya muda.

Taarifa ya kamati ya mashindano ya CAF, imesema kuwa "fataki, mawe, chupa na miale mingine ya moto" ilirushwa uwanjani wakati mechi inaendelea.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kulikuwa na uvamizi wa mashabiki kuingia ndani ya uwanja na kufanya vurugu kubwa baada ya timu yake kuonekana inapoteza mchezo.

Kwa mantiki hiyo, CAF imetangaza kuiondoa mashindanoni klabu ya Setif pamoja na kufuta matokeo ya mchezo kati yake na Mamelodi, hatua ambayo huenda ikaathiri harakati za timu hiyo kufuzu kwenye hatua inayofuata.

Shirikisho la mpira Afrika, CAF, pia limeanza taratibu nyingine za kuchukua hatua zaidi dhidik ya timu hiyo.

Timu nyingine zilizoko kwenye kundi moja wa Mamelodi ni pamoja na Zamalek ya Misri na Enyimba ya Nigeria, ambapo sasa kundi lao litakuwa na timu tatu pekee, huku Zamalek ikiwa kinara kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Enyimba.