OLIMPIKI RIO-IAAF-IOC

IOC yatoa siku 11 kwa wanariadha wa Kenya na Urusi

Vivian Jepkemoi Cheruiyot, mwanariadha wa Kenya.
Vivian Jepkemoi Cheruiyot, mwanariadha wa Kenya. Reuters/Damir Sagolj

Wanariadha wa nchi za Kenya na Urusi, wanaotaka kushiriki kwenye michezo ya Olimpiki ya jijini Rio, Brazil, wametakiwa kuthibitisha ikiwa ni wasafi na wamepewa siku 11 kufanya hivyo.

Matangazo ya kibiashara

Nchi hizi mbili zimefungiwa kushirikia mashindano ya kimataifa kwa kosa la kukiuka sheria zinazokataza matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Hata hivyo kamati ya kimataifa ya Olimpiki, inasema kuwa itawaruhusu wanariadha kushindana kwenye michezo ya Rio, ikiwa tu, watapasi vipimo vya ziada kubaini ikiwa wanatumia dawa za kusisimua misuli au la.

Shirikisho la mchezo wa riadha dunianik IAAF, kupitia kwenye tovuti yake, limechapisha kanuni mpya ambazo zitatumiwa kuthibitisha usafi wa wanamichezo wake, ambapo miongoni mwa kanuni hizo ni pamoja na: -

  • Waombaji wanapaswa kutuma barua pepe kwa katibu mkuu wa IAAf kwa lugha ya Kiingereza, wakiambatanisha ushahidi kuthibitisha kuwa ni wasafi na hawana rekodi za kutumia dawa za kusisimua misuli.
  • Wanamichezo hao pia, watatakiwa kuthibitishwa na maabara zilizoanishwa na WADA, na kwamba maabara hizo zisiwe za Kenya au Urusi.
  • Ushahidi wao unapaswa kutumwa kwa IAAF, kufikia Julai 4, wiki mbili kabla ya muda wa mwisho wa kufuzu kushiriki michezo ya Rio, ambayo ni Julai 18.
  • Wanamichezo watakaohusishwa na makocha waliofungiwa, au kukaa muda mrefu bila kupimwa, au kutoeleweka kwa maeneo yao ya kupatikana, taarifa hizi zitatumika kuwachuja wanamichezo.

 

Hata hivyo nchi za Kenya na Urusi, zimeandika barua kwa kamati ya Olimpiki, IOC, kuomba maelezo zaidi ya namna wanamichezo wao wanaweza kufuzu na wale ambao hawawezi kwaajili ya kushiriki michezo ya Rio.

Katika hatua nyingine, taarifa hiyo haijasema wazi ikiwa wanamichezo watafuzu vipimo hivyo vya ziada wataruhusiwa kushiriki kuziwakilisha nchi zao au la, bado haijulikani.

Rais wa kamati ya Olimpiki, Thomas Bach, amesema wanariadha wa Urusi watakaoonekana kuwa wasafi, wataruhusiwa kushiriki kwa kutumia bendera zao wenyewe na si nchi.

Lakini shirikisho la riadha duniani IAAF, limesema kuwa litawakubali wanariadha ambao watashiriki michezo hiyo kama wanamichezo huru, kwa kutumia bendera ya IOC.