SOKA

Michuano ya kombe la Ulaya yaingia hatua ya mtoano

Mechi iliyopita,  Iceland ikimenyna na  Austria
Mechi iliyopita, Iceland ikimenyna na Austria REUTERS/Charles Platiau

Michuano ya soka kuwania ubingwa wa taji la Ulaya, inaingia katika hatua ya mwondoano leo Jumamosi. 

Matangazo ya kibiashara

Mechi ya kwanza ni kati ya Uswizi na Poland kuanzia saa 10 Kamili saa za Afrika Mashariki.

Timu ya Poland itamkosa kipa wake Wojciech Szczesny anayeuguza jeraha la paja na sasa nafasi yake itachukuliwa na Lukasz Fabianski.

Kiungo wa kati Bartosz Kapustka naye anatarajiwa kukaaa nje baada ya kupata kadi mbili za njano katika mchuano wake wa mwisho.

Wales nao watashuka dimbani kuanzia saa moja jioni kumenyana na Ireland Kaskazini, huku Croatia wakitarajiwa kumenyana na Ureno kuanzia saa nne usiku.

Uswizi ilifuzu katika hatua hii baada ya kumaliza ya pili katika kundi A, nyuma ya wenyeji Ufaransa huku Poland nao wakimaliza wa pili katika kundi la C.

Ireland Kaskazini ilifika katika hatua hii kama mojawapo ya timu bora iliyomaliza nafasi ya tatu katika kundi C, huku Wales wakiongoza kundi B.

Croatia nao wameingia baada ya kuongoza kundi la D kwa kushinda mechi mbili, huku wapinzani wao katika hatua hii Ureno, wakimaliza kati ya timu tatu bora katika kundi F, baada ya kutoka sare mechi zake zote tatu.

Siku ya Jumapili, Ufaransa itachuana na Jamhuri ya Ireland.

Ujerumani dhidi ya Slovakia huku Hungary ikiratibiwa kumenyana na Ubelgiji.