COPA AMERIKA 2016 - MESSI

Messi astaafu soka, huku Argentina ikiangukia pua Copa Amerika

Katika hatua iliyoonekana kuwashanga wapenzi wa soka nchini Argentina na dunia kwa ujumla, mshambuliaji wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, ametangaza kustaafu kuichezea timu yake ya taifa. 

Wachezaji wa timu ya taifa ya Chile, wakishangilia baada ya kukabidhiwa taji la michuano ya Copa Amerika, 26 JUNE 2016
Wachezaji wa timu ya taifa ya Chile, wakishangilia baada ya kukabidhiwa taji la michuano ya Copa Amerika, 26 JUNE 2016 Brad Penner-USA TODAY Sports
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa Messi kustaafu kucheza soka la kimataifa, umewachukua watu kwa mstuko, hasa ikiwa ni baada ya timu yake ya taifa kushindwa kutwaa taji la michuano ya Copa Amerika.

Mchezaji huyo na timu yake ya taifa kwa mara nyingine walishindwa kufua dafu katika ngazi ya kimataifa, ikiwa ni mara ya nne mfululizo kwa mchezaji huyu akiwa na timu yake ya taifa kushindwa kutwaa taji lolote kubwa baada ya hapo jana timu ya taifa ya Chile kuchomoza na ushindi kwa njia ya penati.

"Kwangu mimi, timu ya taifa nimemaliza," alisema Lionel Messi wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi na Chile.

"Nimefanya kila nilichoweza, nimeshiriki fainali nne, inauma kushindwa kuwa bingwa, ni wakati mgumu kwangu na timu nzima pia, na ni ngumu kusema, lakini nimemalizana na timu ya taifa ya Argentina." alisema Messi.

Uamuzi huu wa kushanga wa Lionel Messi umekuja baada ya kushindwa kwenye fainali ya tatu mfululizo akiwa na timu ya taifa, toka kwenye fainali za kombe la dunia nchini Brazil, mwaka 2014.

YALIYOJIRI KATIKA PICHA, FAINALI YA COPA AMERIKA

Argentina ilifungwa bao 1-0 na Ujerumani kwenye fainali ya kombe la dunia mwaka 2014 na kushindwa kwenye hatua ya penati na Chile kwenye fainali ya kombe la Copa Amerika.

Messi pia alishuhudia timu yake ikipoteza kwenye mchezo wa fainali mwaka 2007 ya kombe la Copa Amerika.

Licha ya kutokuwa na mafanikio na timu yake ya taifa, Messi hajapungukiwa kupata mafanikio akiwa na klabu yake ya Barcelona, ambapo ameshinda taji la mchezaji bora wa dunia kwa mara 5.

Licha ya mafanikio haya Messi amekuwa akikosolewa pakubwa na mashabiki wa soka nchini mwake kutokana na kushindwa kuisadia timu yake ya taifa kutwaa mataji muhimu.

Kushindwa kwa Leonel Messi kufikia japo nusu ya rekodi ya mchezaji mkongwe na maarufu nchini humo, Diego Maradona, ambaye bao lake la mkono liliipa taji ya dunia timu yake mwaka 1986, amekuwa akimkosoa mara kadhaa.

Maradona mwenyewe amekuwa akimkosoa Messi kwa kushindwa kuonesha umahiri akiwa na timu ya taifa ukilinganisha na akiwa na timu yake ya Barcelona.