LIVERPOOL - LIGI KUU UINGEREZA

Sadio Mane kujiunga na Liverpool akitokea Southampton

Le Sénégalais Sadio Mané.
Le Sénégalais Sadio Mané. Reuters / Dylan Martinez

Mshambuliaji wa klabu ya Southampton raia wa Senegal, Sadio Mane anatarajiwa kuwa na vipimo vya afya katika klabu ya Liverpool, baada ya timu hizo mbili kukubaliana kuhusu ada ya uhamisho inayodaiwa kuvuka paundi milioni 30.

Matangazo ya kibiashara

Uhamisho huu ukiwa utakamilika, utakuwa ni uhamisho wa gharama kubwa zaidi kuwahi kufanywa na klabu ya Liverpool, na huenda ukazidi dau la paundi za Uingereza milioni 32 wakati wa uhamisho wa mchezaji Christian Benteke na milioni 35 wakati wa uhamisho wa Andy Carroll.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, anataka kuimarisha safu yake ya ushambuliaji na usajili wa Mane ulikuwa ni suala lake la kwanza ambalo aliwaambia viongozi wa Liverpool kuhakikisha wanakamilisha usajili wake.

Inataarifiwa kuwa huenda klabu ya Southampton ilikuwa inataka dau linalokaribia kufikia paundi za Uingereza milioni 40.

Klopp alivutiwa na Mane, wakati mchezaji huyo alipoisaidia timu yake kupata mabao mawili ya haraka na kuipa timu yake ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa ligi kuu uliopigwa Machi 20 mwaka huu.

Akiwa sambamba na mshambuliaji wa Uingereza, Daniel Sturridge na mshambuliaji wa Ubelgiji, Divock Origi, Mane ambaye amefunga mabao 11 kwenye msimu wa ligi iliyomalizika, ataongeza lasi ya safu ya ushambuliaji ya timu ya Liverpool.

Liverpool inatarajiwa kufidia kiasi cha fedha hizo ikiwa watafanikiwa kumuuza mshambuliaji wao, Christian Benteke ambaye hajawa na msimu mzuri toka ajiunge na timu hiyo akitokea Aston Villa.

Mane ataungana na wachezaji wengine waliotoka klabu ya Southampton akiwemo, Adam Lallana, Dejan Lovren, Rickie Lambert na Nathaniel Clyne wote wakijiunga na timu hiyo mwaka 2014.