YANGA-TP MAZEMBE-CAF

Yanga yajigamba kuifunga TP Mazembe, mashabiki kuingia bure

Mashabiki wa klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania, ambao wataingia bure kwenye mchezo wao dhidi ya TP Mazembe.
Mashabiki wa klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania, ambao wataingia bure kwenye mchezo wao dhidi ya TP Mazembe. hivisasa.co.tz

Mechi za hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika CAF zitaendelea tena juma hili kwa michezo minne kupigwa kwa siku tofauti kuanzia Jumanne hadi Alhamisi, Juni 30 ya wiki hii ambapo jijini Dar es Salaam, Tanzania, mabingwa wa soka nchini humo, Yanga watacheza na TP Mazembe ya DRC.

Matangazo ya kibiashara

TP Mazembe ambao waliwahi kuchukua taji la kombe la klabu bingwa barani Afrika ambapo msimu huu walikuwa mabingwa watetezi kabla ya kutupwa nje na kuangukia kwenye kombe la Shirikisho, tayari wamewasili jijini Dar es Salaam.

Mazembe ambao wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na kumbukumbu nzuri ya michuano hii, ambapo mwaka 2013 walifika kwenye hatua ya fainali na kufungwa na klabu ya Tunisia, CS Sfaxien.

Yanga kwa upande wao, walifika kwenye hatua hii ya makundi, baada ya kuondolewa kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya klabu bingwa, wanaingia uwanjani wakiwa hawana historia nzuri ya michuano hii mikubwa barani Afrika.

Afisa habari wa klabu ya Yanga ya Tanzania, Jerry Muro.
Afisa habari wa klabu ya Yanga ya Tanzania, Jerry Muro. RFI

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na idhaa ya Radio France Internationale, RFI, msemaji wa klabu ya Young Africans, Jerry Muro, amesema maandalizi yote ya timu yao, yamekamilika na kwamba wamejiandaa kuhakikisha wanachomoza na ushindi kwenye mchezo huo wa Jumanne, Juni 28, utakaopigwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Katika hatua isiyo ya kawaida, timu hiyo ya Tanzania imesema mashabiki wake wataingia bure uwanjani, ikiwa ni kama sehemu ya kuwalipa fadhila mashabiki wake ambao wamekuwa wakienda na timu hiyo popote inapocheza lakini pia kuhakikisha mashabiki wanakuwa wengi zaidi uwanjani.

Jeshi la Polisi nchini Tanzania, tayari limewatahadharisha mashabiki watakaoenda uwanjani kushuhudia mchezo huo, kuingia kwa utaratibu na kujiepusha na vurugu zozote ambazo zitasababisha Polisi kutumia nguvu, suala ambalo huenda lisiwe na faida kubwa kwa Yanga kutokana na sheria mpya za CAF zinazosmamia mashindano haya.

Mechi nyingine ambazo zitachezwa juma hili ni pamoja na Al Ahli Tripoli ya Libya itakayopepetana na Kawkab Marrakech ya Morocco, mchezo ambao utachezwa Jumanne, ya wiki hii.

Siku ya Jumatano, Medeama ya Ghana itakuwa nyumbani kucheza na Mo Bejaia ya Algeria, wakati Alhamisi Juni 30, Etoile du Sahel ya Tunisia, itacheza na FUS Rabat ya Morocco.