CAF-SOKA

TP Mazembe yaiachia Yanga kilio

Wachezaji wa TP Mazembe wakisherehekea ushindi
Wachezaji wa TP Mazembe wakisherehekea ushindi static.goal.com

Klabu ya soka ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imepata ushindi muhimu wa bao 1 kwa 0 dhidi ya Yanga FC ya Tanzania katika mchuano wa pili wa hatua ya makundi kutafuta ubingwa wa taji la Shirikisho barani Afrika.

Matangazo ya kibiashara

Mechi hiyo imechezwa leo Jumanne katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam iliyohudhuriwa na maelfu ya mashabiki kwa sababu mechi hiyo ilikuwa bure na uwanja ulianza kufurika kuanzia asubuhi.

Bao hilo la Mazembe lilifungwa na mchezaji Merveille Bokadi katika dakika ya 74 kipindi cha pili baada ya kupata pasi murua kutoka kwa mchezaji mwenzake Roger Assale.

Mazembe walipata nafasi hiyo ya kipekee ya kupata bao baada ya mshambuliaji wake raia wa Tanzania, Thomas Ulimwengu kuangushwa katika eneo la hatari na refarii Janny Sikwaze kutoka Zambia kuwapa mkwaju wa adhabu.

Kwa matokeo haya, TP Mazembe inaendelea kuongoza kundi la A kwa alama 6, baada ya kushinda mechi yake ya kwanza dhidi ya Medeama ya Ghana kwa mabao 3 kwa 1 wiki mbili zilizopita.

Yanga haina alama yoyote kwa sababu mechi yake ya kwanza ilifungwa na Mo Bejaia ya Algeria bao 1 kwa 0.

Mechi ijayo Yanga wataikaribisha Medeama ya Ghana huku TP Mazembe ikisafiri kwenda ugenini kumenyana na MO Bejaia katikati ya mwezi ujao wa Julai.