IBRAHIMOVIC-MAN UTD-EPL

Ibrahimovic kukamilisha usajili wake na Man United mwishoni mwa juma

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic REUTERS/Stephane Mahe

Taarifa za ndani ya klabu ya Manchester United zinasema kuwa mshambuliaji wa kimataifa wa Sweden aliyetangaza kustaafu kucheza soka la kimataifa, Zlatan Ibrahimovic huenda akakamilisha usajili wa kujiunga na timu hiyo mwishoni mwa juma. 

Matangazo ya kibiashara

Zlatan mwenye umri wa miaka 34 hivi sasa, yuko huru baada ya kuachana na klabu ya PSG ya nchini Ufaransa, na anatarajiwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya Old Trafford.

Ikiwa makubaliano yatakamilika ndani ya muda, Zlatan atakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na kocha mpya wa timu hiyo, Mreno, Jose Mourinho, aliyechukua nafasi ya Louis van Gaal kuwa kocha mkuu mwezi May.

Tayari beki wa kati raia wa Ivory Coast, Eric Bailly mwenye umri wa miaka 22, ameshakamilisha usajili wake wa kujiunga na klabu hiyo kwa dau la paundi za Uingereza milioni 30 akitokea timu ya Villarreal ya Uhispania.

Zlatan Ibrahimovic, akiaga mashabiki wa PSG wakati wa mechi yake ya mwisho kuichezea timu hiyo ya Ufaransa, 2016
Zlatan Ibrahimovic, akiaga mashabiki wa PSG wakati wa mechi yake ya mwisho kuichezea timu hiyo ya Ufaransa, 2016 REUTERS/Gonzalo Fuentes

United pia, imeboresha ofa yake ya kutaka kumnasa mchezaji, Henrikh Mkhitaryan mwenye umri wa miaka 27, na sasa wanasubiri klabu yake ya Borussia Dortmund iamue hatma ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Armenia.

Ibrahimovic aliondoa kikwazo kilichokuwepo awali cha kuhamia kucheza kwenye timu za Uingereza, baada ya kutangaza kuwa hatoenda kushiriki michezo ya Olimpiki ya Rio ya mwaka huu, kufuatia timu yake kuondolewa kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya kombe la Ulaya 2016.

Itakuwa ni mara yake ya kwanza kucheza ligi ya Uingereza, baada ya kutwaa mataji kadhaa akiwa na timu tofauti barani Ulaya.

Ibrahimovic alikuwa mfungaji kwenye ligi kuu ya Ufaransa, Ligue 1 msimu uliopita akiwa na magoli 38, lakini hakufunga bao lolote hadi Sweden ikitolewa kwenye michuano ya Ulaya.