EURO 2016

Ronaldo: Mechi dhidi ya Poland ni yakufa na kupona

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, akijaribu kumiliki mpira kifuano wakati wa mazoezi ya timu yake.
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, akijaribu kumiliki mpira kifuano wakati wa mazoezi ya timu yake. MIGUEL A. LOPES/LUSA

Mechi ya robo fainali ya kwanza ya michuano ya kombe la mataifa Ulaya, inatarajiwa kupigwa Alhamisi ya wiki hii, Juni 30, kwa timu ya taifa ya Poland itakayokuwa na kibarua dhidi ya Ureno.

Matangazo ya kibiashara

Poland ilifika kwenye hatua hii ya robo fainali baada ya kuifunga timu ya taifa ya Uswisi katika mchezo wa hatua ya 16 bora, ulioamuliwa kwa njia ya Penati, ambapo ilikuwa ni timu ya kwanza kutinga robo fainali.

Ureno kwa upande wao, baada ya kuponea chupuchupu kwenye hatua ya makundi na kuingia hatua ya 16 bora kama mshindi wa tatu bora kwenye kundi lake, ilifanikiwa kufika hatua ya robo fainali baada ya kuchomoza na ushindi dhidi ya Croatia, bao likifungwa kwenye muda wa dakika 30.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid ya Uhispania, Christian Ronaldo, anasema mchezo wao dhidi ya Poland utakuwa ni miongoni mwa michezo migumu zaidi waliyowahi kucheza kwenye michuano ya Ulaya.

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Poland, Adam Nawalka.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Poland, Adam Nawalka. REUTERS/UEFA/Handout

Ronaldo anasema mchezo dhidi ya Poland utakuwa mgumu, lakini wamejipanga kuhakikisha wanachomoza na ushindi na kuingia kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya mwaka huu, kitu ambacho mwenyewe anasema ndicho anachotaka.

Mabeki wa kati wa timu ya taifa ya Poland, Michal Pazdan na Kamil Glik wamekiri mtihani ulioko mbele yao, ambao ni wa kuhakikisha wanamdhibiti kwa dakika zote tisini mshambuliaji wa Ureno, Christian Ronaldo ambaye wanasema atawasumbua.

Glik anasema katika historia yake amecheza na washambuliaji wengi na kuwadhibiti lakini anakiri kuwa na kazi ngumu ya kumdhibiti kwa dakika zote 90, Christian Ronaldo, anayesema atakuwa chachu ya ushindi ya Ureno.