UINGEREZA - FA

Southgate huenda akapewa kwa muda mikoba ya Hodgson

Kocha wa timu ya taifa ya vijana ya Uingereza, chini ya umri wa miaka 21, Gareth Southgate.
Kocha wa timu ya taifa ya vijana ya Uingereza, chini ya umri wa miaka 21, Gareth Southgate. DR

Chama cha soka nchini Uingereza, kinajiandaa kumtangaza kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 21, Gareth Southgate, kuwa kocha wa muda wa timu ya taifa inayojiandaa na mechi za kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia nchini Urusi, mwaka 2018.

Matangazo ya kibiashara

FA inahaha kumtafuta mrithi wa aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson ambaye alitangaza kubwaga manyanga kukinoa kikosi hicho, mara baada ya timu yake kutolewa kwenye hatua ya 16 bora na Iceland.

Mkurugenzi mtendaji wa shirikisho la soka nchini humo, FA, Martin Glenn, akiwa ameketi sambamba na Hodgson, alisema uteuzi wa kumpata kocha mpya utachukua muda zaidi na utachukua hata miezi kabla ya kumpata.

Waandishi wa habari waligusia kuhusu uwezekano wa kuteuliwa kwa kocha mkuu wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger, kuwa kocha mkuu wa Uingereza, Glenn, hakukubali wala kuktaa uwezekano huo, wakati huu Wenger akiwa amebakiza mwaka mmoja tu kwenye mkataba wake.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kocha wa vijana chini ya umri wa miaka 21 kuiongoza timu hiyo kwenye mchezo wa kwanza wa kufuzu dhidi ya Slovakia mwezi September, alisema "Tutaona.

"Tunatamani kupata kocha atakayeongoza kikosi chetu kwenye mechi za kufuzu, lakini kama tusipompata mapema, basi tayari tunae mtu wa kuiongoza timu kwa muda." alisema Glenn.

Aliongeza kuwa uteuzi wa kocha mpya, utafanywa na mkurugenzi mtendaji Glenn, akisaidiwa na mjumbe wa bodi ya FA, David Gill na mkurugenzi wa ufundi, Dan Ashworth, na wanatarajiwa kuanza mazungumzo ya kupitia majina ambayo wanadhani wanaweza kuchukua nafasi hiyo.