HISPANIA-DEL BOSQUE-IBRAHIMOVIC

Del Bosque atangaza kubwaga manyanga, Ibrahimovic kutua Man Utd

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Hispania, Vicent de Bosque ambaye ametangaza kujiuzulu nafasi yake kwenye timu ya taifa.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Hispania, Vicent de Bosque ambaye ametangaza kujiuzulu nafasi yake kwenye timu ya taifa. REUTERS/Michael Dalder/File Photo

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente del Bosque, ametangaza kujiuzulu nafasi yake kwenye kikosi hicho, baada ya kushuhudia timu yake ikitupwa nje kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya Ulaya na Italia.

Matangazo ya kibiashara

Del Bosque, mwenye umri wa miaka 65, aliiongoza Hispania kutwaa taji la kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, taji la kwanza kwenye hostoria yake, na pia kutwaa mataji mfululizo ya kombe la Ulaya mwaka 2012.

Kocha huyo alichukua nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Luis Aragones aliyeiongoza Hispania kutwaa taji la Ulaya mwaka 2008.

Akuzungumza na kituo kimoja cha redio nchini Hispania, del Bosque anasema "Sina lengo lolote la kusalia kuwa kocha mkuu tena."

Kocha huyo ameongeza kuwa, uamuzi huu alishaufikia hata kabla ya kuanza kwa michuano ya Ulaya na kujua hatma yake kwenye mashindano ya mwaka huu, na kwamba kwa vyovyote vile angejiuzulu baada ya kumalizika kwa michuano ya mwaka huu.

Del Bosque aliwasilisha barua ya kujizulu nafasi yake baada ya fainali za kombe la dunia mwaka 2014, lakini alishawishiwa na wakuu wa shirikisho la soka nchini humo na kuamua kubakia.

Hispania ilishinda mchezo wake wa kwanza kombe la Ulaya mwaka huu kwa kuifunga Jamhuri ya Czech na Uturuki lakini ikajikuta ikila kichapo toka kwa Croatia na kumaliza kwenye nafasi ya pili kwenye kundi D na kukutana na Italia kwenye hatua ya 16 bora.

Zlatan Ibrahimovic, mshambuliaji wa Sweden aliyeweka wazi kuwa atajiunga na Manchester United
Zlatan Ibrahimovic, mshambuliaji wa Sweden aliyeweka wazi kuwa atajiunga na Manchester United REUTERS/Christian Hartmann Livepic

Katika hatua nyingine mchambuliaji wa kimataifa wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic, baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu kuhusu hatima yake kisoka, jana amevunja ukimya hio baada ya kuandika kwenye ukurasa wake wa kijamii kuwa atajiunga na klabu ya Manchester United.

Ibrahimovic amekuwa akihusishwa na kujiunga na Manchester United toka alipotangaza kuachana na klabu ya PSG ya nchini Ufaransa.