EURO 2016

Ureno yatinga nusu fainali, leo ni Wales au Ubelgiji

Cristiano Ronaldo wa Ureno akishangilia baada ya timu yake kuvuka hatua ya robo fainali na sasa kucheza nusu fainali kombe la Ulaya.
Cristiano Ronaldo wa Ureno akishangilia baada ya timu yake kuvuka hatua ya robo fainali na sasa kucheza nusu fainali kombe la Ulaya. MIGUEL A. LOPES/LUSA

Mechi za robo fainali za michuano ya kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 2016, zimeanza kupigwa Alhamisi ya wiki hii, ambapo timu ya taifa ya Ureno imekuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya nusu fainali.

Matangazo ya kibiashara

Alhamisi, Juni 30, timu ya taifa ya Ureno walikuwa wakichuana na Poland kwenye mchezo wa robo fainali, mechi ambayo ilikuwa ya aina yake kutokana na kosa kosa nyingi za wachezaji wa pande zote mbili.

Poland waliingia kwenye mchezo huo kwa lengo la kutaka kutengeneza historia huku Ureno, baada ya kushiriki kwenye michuano kadhaa ya Ulaya bila kupata taji lolote, waliingia uwanjani kwa lengo moja tu la kupata ushindi.

Hata hivyo dakika 90 zilishuhudia timu hizo zikimalizika kwa sare ya bao 1-1, ambapo mchezo huo ulilazimika kwenda kwenye muda wa nyongeza wa dakika 30.

Muda wa nyongeza pia haukutosha kwa timu moja kuibuka na ushindi, hali iliyolazimu mchezo huo kumalizwa kwa njia ya penati ili kupata mshindi atakayecheza hatua ya nusu fainali.

Kwenye hatua hiyo, Ureno walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa penati 5 - 3 dhidi ya Poland, huku mshambuliaji wa Ureno, Christian Ronaldo akiifungia timu yake penati baada ya mkwaju wa mwisho aliopiga kwenye hatua ya 16 bora kupanguliwa na mlinda mlango.

Hivi leo mchezo mwingine wa robo fainali utapigwa, ambapo Wales watakuwa wanacheza na Ubelgiji, kwenye mchezo ambao tayari umevuta hisia za maelfu wa mashabiki duniani.

Wales wanawategemea wachezaji wake Gareth Bale na Aaron Ramsey kuongoza mashambulizi yao, huku kwa Ubelgiji, wao wakiwategemea wachezaji kama vile Romelu Lukaku na nahodha Edin Hazard ambao wamekuwa chachu ya ushindi kwa timu yao.