EPL-MANUTD

Dortmund yakubali dau la Man Utd, kuhusu usajli wa Mkhitaryan

Henrikh Mkhitaryan, mshambuliaji wa Borussia Dortmund anayetarajiwa kujiunga na Manchester United ya Uingereza
Henrikh Mkhitaryan, mshambuliaji wa Borussia Dortmund anayetarajiwa kujiunga na Manchester United ya Uingereza REUTERS/Ina Fassbender

Klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani, hatimaye imekubali ofa ya usajili wa mshambuliaji wake, Muarmenia, Henrikh Mkhitaryan, anayetakiwa na klabu ya Uingereza, Manchester United. 

Matangazo ya kibiashara

Nahodha huyu wa timu ya taifa ya Armenia, aliigharimu klabu hiyo ya Ujerumani, Paundi za Uingereza milioni 23.5 wakati akisajiliwa na timu hiyo mwaka 2013, na alikuwa anamaliza mkataba wake mwaka msimu ujao.

"Kama tungekataa ofa hii, mchezaji huyu angekuwa huru mwaka 2017," amesema mkurugenzi mkuu wa Dortmund, Hans-Joachim Watzke, kupitia mtandao wa klabu hiyo.

Mkhitaryan, mwenye umri wa miaka 27 hivi sasa, wakati wowote anatarajiwa kuwa na vipimo vya afya kwenye klabu ya Manchester United, ambapo pia makubaliano kadhaa binafsi na timu hiyo bado hayajakamilika.

Ikiwa makubaliano yatafikiwa, atatakiwa kupata hati ya kufanyia kazi nchini Uingereza na atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Manchester United msimu huu, baada ya usajili wa Muaivory Coast, Eric Bailly na mshambuliaji wa kimataifa wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, alimsajili Mkhitaryan kutoka klabu ya Ukraine ya Shakhtar Donetsk, wakati huo akikinoa kikosi cha Dortmund.

Mkhitaryan, alitajwa kuwa mchezaji bora wa msimu wa ligi kuu ya Bundesliga msimu wa mwaka 2015-2016, baada ya kufunga mabao 18 kwenye mashindano yote, likiwemo bao moja dhidi ya Liverpool kwenye michuano ya Europa League, kwenye uwanja wa Anfield.

Mkhitaryan, ni mtoto wa mchezaji maarufu wa zamani wa Armenia, Hamlet Mkhitaryan.