EURO 2016

Euro 2016: Nusu fainali ya kufa na kupona kuweka historia

Mashabiki wakiwapongeza wachezaji wao wa timu ya taifa ya Iceland
Mashabiki wakiwapongeza wachezaji wao wa timu ya taifa ya Iceland REUTERS/John Sibley Livepic

Hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la mataifa ya Ulaya “Euro 2016” imemalizika mwishoni mwa juma, ambapo miamba iliyofuzu kwenye hatua ya nusu fainali, imejulikana na mechi zitapigwa siku ya Jumatano na Alhamisi ya wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Alhamisi ya wiki iliyopita, Juni 30, ilishuhudiwa timu ya taifa ya Ureno ikifuzu kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya mwaka huu baada ya kupata ushindi dhidi ya timu ya taifa ya Poland, mtanange ambao uliamuliwa kwa njia ya Penati, baada ya kumalizika kwa muda wa nyongeza wa dakika 30, timu hizo zikiwa sare ya bao 1-1.

Wachezaji wa Iceland wakitoa heshima kwa mashabiki wao baada ya mchezo dhidi ya Ufaransa ambapo walipoteza kwa mabao 5-2
Wachezaji wa Iceland wakitoa heshima kwa mashabiki wao baada ya mchezo dhidi ya Ufaransa ambapo walipoteza kwa mabao 5-2 REUTERS/Christian Hartmann Livepic

Siku ya Ijumaa, Julai Mosi, mchezo mwingine wa robo fainali ulipigwa, ambapo timu ya taifa ya Wales ilicheza na timu ya taifa ya Ubelgiji, kwenye mchezo ambao ulishuhudia Wales wakiweka historia baada ya kufuzu kwa mara ya kwanza kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano mikubwa duniani kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kwa matokeo ya mechi za Alhamisi na Ijumaa, yanamaanisha kuwa, sasa mechi ya kwanza ya nusu fainali ya michuano ya kombe la Ulaya, itazikutanisha timu ya taifa ya Ureno ambayo itakuwa inasaka nafasi ya kutinga hatua ya fainali, itakapocheza na Wales, ambao ni mara yao ya kwanza kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano mikubwa duniani.

Wachezaji wa Italia wakiwa wameinamisha vichwa chini baada ya kushindwa dhidi ya Ujerumani kupitia njia ya penati
Wachezaji wa Italia wakiwa wameinamisha vichwa chini baada ya kushindwa dhidi ya Ujerumani kupitia njia ya penati REUTERS/Darren Staples Livepic

Jumamosi, Julai 2, timu ya taifa ya Ujerumani ilifanikiwa kutinga kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya mwaka huu, baada ya kufanikiwa kuchomoza na ushindi dhidi ya timu ya taifa ya Italia, mchezo ambao haya hivyo ilibidi uamuliwe kwa njia ya penati baada ya timu hizo kwenda sare ya bao 1-1 hadi kwenye muda wa nyongeza wa dakika 30.

Siku ya Jumapili, Julai 3, wenyeji wa michuano ya mwaka huu, timu ya taifa ya Ufaransa, yenyewe ilikuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Iceland ambayo nayo ilifika kwenye hatua hii kwa kuweka historia baada ya kuifunga timu ya taifa ya Uingereza kwenye hatua ya 16 bora.

Kwenye mchezo huu ambao timu mwenyeji Ufaransa haikuwa na huruma hata kidogo kwa Iceland, ilitoa kipigo mfano wa mbwa mwizi, baada ya kuicharaza timu hiyo kwa jumla ya mabao 5-2, kwenye mchezo ambao kwa sehemu kubwa ulitawaliwa na na wenyeji Ufaransa.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani wakishangilia baada ya kupata ushindi wa njia ya penati dhidi ya Ufaransa mwishoni mwa juma
Wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani wakishangilia baada ya kupata ushindi wa njia ya penati dhidi ya Ufaransa mwishoni mwa juma REUTERS/Darren Staples Livepic

Kwa matokeo ya mechi za mwishoni mwa juma, ni wazi sasa, mabingwa wa dunia timu ya taifa ya Ujerumani, itacheza dhidi ya wenyeji wa michuano ya mwaka huu, Ufaransa, katika mchezo wa nusu fainali ambao tayari umevuta hisia kubwa za mashabiki wa soka.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa wakishangilia mara baada ya mchezo wao dhidi ya Iceland
Wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa wakishangilia mara baada ya mchezo wao dhidi ya Iceland REUTERS/Darren Staples Livepic

Mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya michuano ya kombe la Ulaya 2016, utachezwa siku ya Jumatano, Julai 6, ambapo timu ya taifa ya Ureno itakuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Wales, kwenye mchezo ambao na wenyewe umevuta hisia za mashabiki wengi wa soka.

Ureno watecheza mchezo huu, huku wakiwa hawana kumbukumbu nzuri ya matokeo yaliyowafanya mpaka wamefikia hatua hii, kwakuwa hata uchezaji wao licha ya kumtegemea mshambuliaji wake wa kimataifa Christian Ronaldo hawakuwa tishio sana msimu huu.

Mshambuliaji na winga wa timu ya taifa ya Ureno, Luis Nani, akimiliki mpira wakati wa mazoezi ya timu yake
Mshambuliaji na winga wa timu ya taifa ya Ureno, Luis Nani, akimiliki mpira wakati wa mazoezi ya timu yake REUTERS/John Sibley

Ureno watakuwa wanamtegemea Ranaldo na Luis Nani kuongoza mashambulizi, huku safu ya kiungo wakimtegemea kinda Sanchez ambaye ameonekana kuwa mwiba mkubwa kwa timu pinzani.

Wales wenyewe watacheza mchezo huu huku wakiwa na kumbukumbu nzuri ya matokeo yaliyowawezesha kufika kwenye hatua hii ya nusu fainali, baada ya ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Ubelgiji.

Wales inawategemea wachezaji, Gareth Bale na Aaron Ramsey kuongoza mashambulizi ya timu yao.