LIONEL MESSI-FC BARCELONA

Lionel Messi ahukumiwa kifungo cha miezi 21 jela kwa kosa la ukwepaji kodi

Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi akiwa mahakamani pamoja na baba yake Jorge Messi, wawili hawa wamehukumiwa kifungo gerezani kwa makosa ya ukwepaji kodi
Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi akiwa mahakamani pamoja na baba yake Jorge Messi, wawili hawa wamehukumiwa kifungo gerezani kwa makosa ya ukwepaji kodi REUTERS/Alberto Estevez/Pool/Files

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina na klabu ya FC Barcelona ya nchini Hispania, Lionel Messi, amehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela kwa makosa ya ukwepaji kodi, vyombo vya habari vya Hispania vimeripoti.

Matangazo ya kibiashara

Baba yake, Jorge Messi, pia alihukumiwa kutumikia kifungo jela kwa makosa ya ubadhilifu wa euro milioni 3.5 na milioni 4.5 kati ya mwaka 2007 na 2009.

Mwanandinga huyo pamoja na baba yake, pia wametakiwa kulipa fidia ya mamilioni ya Euro kwa ukwepaji kodi na kuficha fedha kwenye nchi za Belize na Uruguay, fedha ambazo walizipata kutokana na haki za kutumia picha yake.

Mshambuliaji wa FC Barcelona, Lionel Messi, ambaye amehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela
Mshambuliaji wa FC Barcelona, Lionel Messi, ambaye amehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela Reuters/Toby Melville

Hata hivyo, wataalamu wa sheria nchini Hispania, wanasema kuwa huenda wasitumikie kifungo gerezani, kwakuwa sheria za Hispania, zinasema wazi kuwa, mtu akihukumiwa kifungo cha chini ya miaka miwili, anaweza asitumikie kifungo hicho jela na badala yake kuwa chini ya uangalizi maalumu.

Lionel Messi na baba yake walipatikana na hatia ya makosa matatu ya ukwepaji kodi, katika uamuzi uliosomwa kwenye mahakama ya mjini Barcelona.

Wakati wa kesi hiyo, Lionel Messi aliiambia mahakama kuwa, hakufahamu chochote kuhusu fedha zilizopatikana kupitia njia ya matangazo na usajili wake, na kwamba masuala yote yaliyokuwa yakihusu matumizi ya fedha zake, baba yake ndiye alikuwa muhusika mkuu.