SERIA A - AC MILAN

Silvio Berlusconi aiuza klabu yake ya AC Milani kwa Wachina

Wachezaji wa AC MIlan akishangilia taji la ubingwa wa Ulaya, wakati walipowahi kulishinda
Wachezaji wa AC MIlan akishangilia taji la ubingwa wa Ulaya, wakati walipowahi kulishinda DR

Waziri mkuu wa zamani wa Italia na mmiliki wa klabu ya mpira wa miguu ya AC Milani, inayoshiriki ligi kuu ya Seria A, Silvio Berlusconi, ametangaza kuiuza klabu hiyo kwa kampuni ya wachina.

Matangazo ya kibiashara

Berlusconi alitoa matamshi haya wakati alipohojiwa na gazeti moja la kila siku, ambapo alisema kampuni hiyo ya wachina, italipa Euro milioni 220 katika kipindi cha miaka miwili ijayo, ambapo kwa tathmini yao klabu hiyo itawagharimu paundi za Uingereza milioni 750 yakiwemo madeni ya klabu hiyo.

Bila ya kuitaja kampuni iliyonunua klabu hiyo, Berlusconi ameliambia gazeti hilo kuwa, hatimaye amefikia uamuzi wa kuiuza timu yake kwa matajiri wa kutoka China.

Hata hivyo licha ya yeye mwenyewe kusema ameshaiuza klabu hiyo, vyanzo vya ndani vya mwanasiasa huyo, vinasema kuwa kuna mazungumzo bado yanaendelea na yaikamilika itatangazwa rasmi.

Berlusconi mwenye umri wa miaka 79, alihudumu kama waziri mkuu wa Italia kwa mara nne, lakini alihukumiwa kwenda jela kwa makosa ya ukwepaji kodi na rushwa.

Waziri mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi
Waziri mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi REUTERS/Flavio Lo Scalzo

Kampuni ya familia yake "Fininvest" imeripotiwa kuwa iliingia kwenye mazungumzo na wawekezaji hao kutoka China, mwezi May mwaka huu.

Kampuni hiyo inaelezwa kuwa, itanunua asilimia 80 ya klabu hiyo kabla ya kumalizia kiasi chote kilichobakia baada ya kuwa na umiliki.

AC Milan, moja ya klabu kubwa barani Ulaya na iliyowahi kupata mafanikio makubwa, inajaribu kutafuta uwekezaji mkubwa zaidi ili kuifanya kuwa miongoni mwa timu zitakazoleta ushindani tena barani Ulaya na kushindana na wapinzani wake ambao wana wawekezaji wakubwa.

Mwaka jana klabu hiyo ilirekodi hasara ya Paundi za Uingereza milioni 93.5.

Mwaka jana pia, Berlusconi alimanusura aiuze klabu hiyo kwa tajiri kutoka Thailand, lakini baadae akabadili mawazo.

Klabu nyingi barani Ulaya, hivi sasa zinamilikiwa na matajiri kutoka Asia na makampuni kutoka Asia Mashariki.

Klabu pinzani yake, Inter Milan, mwezi uliopita iliuzwa kwa kampuni ya masuala ya kielektriniki kutoka China.

Na mwezi uliopita pia, tajiri kutoka China, Dr Tony Xia alihitimisha ununuzi wa klabu ya Aston Villa ya Uingereza kwa Paundi milioni 76.