EURO 2016

Wales kusaka historia dhidi ya Ureno

Uwanja wa Stade de Lyon nchini Ufaransa
Uwanja wa Stade de Lyon nchini Ufaransa Uefa

Timu ya taifa ya mchezo wa soka ya Wales inajiadaa kucheza mchezo wa kihistoria hivi leo dhidi ya Ureno katika mchuano wa kwanza wa nusu fainali kuwania taji la bara Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Mchuano huo utachezwa usiku huu kuanzia saa nne usiku saa za Afrika Mashariki katika uwanja wa Stade de Lyon mjini Lyon,  nchini Ufaransa.

Hii ndio mara ya kwanza kwa Wales ambayo sasa inafunzwa na kocha Chris Coleman kufika katika hatua hii kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1958.

Kocha Coleman amekuwa akisema wiki hii kuwa anafahamu kuwa wengi wanaona kuwa timu yake ni ndogo na haina majina makubwa lakini inakwenda kupambana uwanjani.

Mshambuliaji Gareth Bale anategemewa sana kuongoza mashambulizi kuelekea lango la Ureno.

Bale atakutana na mchezaji mwezake Christiano Ronaldo wa Ureno wanaocheza pamoja katika klabu ya Real Madrid nchini Uhispania.

Mashabiki wa soka dunia watakuwa wanaangalia wachezaji hawa kwa karibu wakiwa na imani na kuona nani atamzidi mwenzake.

Maelfu ya mashabiki wa Wales wamewasili nchini Ufaransa kwa usafiri wa basi  kwenda kuishabikia timu yao, kushuhudia historia.

Kuelekea kwenye hatua hii, Wales walishinda mechi mbili kati ya tatu walizocheza katika hatua ya makundi.

Hatua ya 16 bora iliishinda Ireland Kaskazini bao 1 kwa 0 na baadaye kuiangusha Ubelgiji kwa mabao 3 kwa 1.

Ureno haikushinda mchuano wowote katika hatua ya makundi na badala yake kupata sare katika mechi zake zote tatu.