EURO 2016

Ujerumani na Ufaransa kujua hatima yao, Ureno yatinga fainali

Wachezaji wa Ureno wakishangilia baada ya mchezo wao dhidi ya Wales kumalizika na wao kutinga hatua ya fainali baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0.
Wachezaji wa Ureno wakishangilia baada ya mchezo wao dhidi ya Wales kumalizika na wao kutinga hatua ya fainali baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0. REUTERS/Carl Recine

Michuano ya kombe la mataifa ya Ulaya 2016, imeendelea kutimua vumbi nchini Ufaransa, ambapo sasa imefikia hatua ya nusu fainali, huku Ureno ikiwa timu ya kwanza kufuzu kucheza fainali ya mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Ureno walipata nafasi hiyo, baada ya hapo jana kufanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wales, ambao walikuwa wanatarajia kutengeneza historia ya kipekee kwa kucheza fainali ya mwaka huu.

Ureno walipata bao lao la kwanza katika dakika ya 50 ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wake na nahodha wa timu hiyo, Christian Ronaldo ambaye alifunga kwa kichwa, kabla ya Luis Nani kuifungia timu yake bao la pili na la ushindi katika dakika ya 53 ya mchezo.

Kwenye mchezo huu, ambao Ureno walikuwa hawapewi nafasi sana dhidi ya Wales, mambo yalikuwa tofauti, kwani ni Ureno ambao walionekana kuwa na njaa zaidi ya kutafuta mabao na kutinga kucheza hatua ya fainali, kitu ambacho wamefanikiwa.

Nahodha wa Wales, Gareth Bale akipiga makofi kuwashukuru mashabiki wa timu yao, baada ya kupoteza dhidi ya Ureno kwenye hatua ya nusu fainali.
Nahodha wa Wales, Gareth Bale akipiga makofi kuwashukuru mashabiki wa timu yao, baada ya kupoteza dhidi ya Ureno kwenye hatua ya nusu fainali. Reuters

Nahodha wa Wales, Gareth Bale, mara baada ya mchezo, aliwashukuru mashabiki wa timu yao, na kusisitiza kuwa timu yao haina cha kujutia katika ushiriki wao wa michuano ya mwaka huu wala kupoteza mchezo dhidi ya Ureno, kwakuwa kile walichokuwa wanakitaka kwenye michuano ya mwaka huu walikifanikisha kwa asilimia 99.

Hivi leo nusu fainali ya pili itacheza katika dimba la Stade de France, ambapo wenyeji Ufaransa watakuwa na kibarua dhidi ya mabingwa wa dunia timu ya taifa ya Ujerumani, mchezo ambao tayari umeanza kuwapandisha presha mashabiki wa timu zote mbili.

Ujerumani wanataka kutengeneza historia kama waliyowahi kuitengeneza timu ya taifa ya Hispania kwa kuchukua taji la dunia na lile la Ulaya mfululizo, huku Ufaransa ikitaka kuweka historia ya kulibakiza kombe hilo kwenye ardhi yake ya nyumbani.