SUDAN KUSINI-ATLABARA FC

Viongozi wawili wa timu ya Atlabara FC ya Sudan Kusini wauawa kwenye mapigano

Wwachezaji wa timu ya Atlabara ya Sudan Kusini ambayo imepoteza viongozi wake wawili kwenye mapigano
Wwachezaji wa timu ya Atlabara ya Sudan Kusini ambayo imepoteza viongozi wake wawili kwenye mapigano DR

Maofisa wawili kutoka Sudan Kusini ambao walikuwa viongozi wa mabingwa wa soka nchini humo, klabu ya Atlabara, wameuawa kwenye mapigano mapya yaliyozuka nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Viongozi hao, William Batista na Leko Nelson, walinaswa kwenye mapigani mjini Juba, kati ya vikosi vya Rais Salva Kiir na wale wa waasi wa Riek Machar, mwishoni mwa juma.

Batista yeye alikuwa katibu mkuu na Nelson alikuwa ni meneja wa timu hiyo.

Chama cha soka nchini Sudan Kusini, kupitia rais wake, Chabur Goc, amethibitisha kuuawa kwa viongozi hao na kuandika kwenye mtandao wa chama hicho kuwa "Tumepoteza marafiki zeru wawili kwenye soka, na mungu azilaze roho zao mahala pema peponi".

Vikosi vya Rais Salva Kiir na vile vya makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar, vilianza kukabiliana mwishoni mwa juma lililopita mjini Juba.

Uhusiano baina ya wakuu wa nchi ya Sudan Kusini, haujawa mzuri sana toka taifa hilo lijitenge na utawala wa Khartoum mwaka 2011.