UGANDA - BESIGYE

Kizza Besigye aachiwa kwa dhamana na mahakama kuu Uganda

Mahakama kuu nchini Uganda, imemuachia kwa dhamana kiongozi mkuu wa upinzani na aliyekuwa mgombea Urais kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Dr. Kizza Besigye. 

Kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye akisindikizwa na maofisa wa gereza la Luzira alikokuwa akishikiliwa kabla ya leo, Julai 12 kuachiwa kwa dhamana na mahakama kuu
Kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye akisindikizwa na maofisa wa gereza la Luzira alikokuwa akishikiliwa kabla ya leo, Julai 12 kuachiwa kwa dhamana na mahakama kuu DR
Matangazo ya kibiashara

Mwanasiasa huyo wa chama cha The Forum for Democratic Change, FDC, alikuwa anazuiliwa kwenye gereza la Luzira akituhumiwa kwa kosa la uhaini.

Akitoa uamuzi wake, Jaji Wilson Masalu Musene, amesema kuwa dhamana anayopewa Besigye ni ishara ya haki ya kisheria ya mtuhumiwa, ya kwamba hana hatia hadi pale atakapopatikana na hatia au mtu kukiri kosa.

Jaji Masalu ameongeza kuwa "kipekee Besigye kama watuhumiwa wengine, alikuwa anahudhuria vikao vya kesi yake kwa uaminifu".

Besigye, mgombea wa nafasi ya Urais kwa zaidi ya mara nne na kushika nafasi ya pili kwenye chaguzi zote, mwezi February mwaka huu baada tu ya kumalizika kwa uchaguzi wa rais, alijiapisha ambapo baadae alishtakiwa kwa kosa la uhaini.

Kwa mujibu wa sheria za Uganda, kifungu namba 23 cha Penal Code, kinasema kuwa, mtu akipatikana na hatia ya kosa la uhaini, hukumu yake ni adhabu ya kifo.

Makosa mengine yanayomkabili Besigye ni pamoja na kujitangaza mshindi kinyume cha sheria, kukaidi amri halali ya polisi na kuitisha maandamano kinyume cha sheria pamoja na kula kiapo kinyume na sheria za nchi.