CAF

Yanga FC kusaka ushindi muhimu dhidi ya Medeama ya Ghana

cafonline

Michuano ya soka hatua ya makundi kuwania taji la klabu bingwa na Shirikisho inachezwa katika viwanja mbalimbali barani Afrika mwishoni mwa juma hili.

Matangazo ya kibiashara

Klabu ya Yanga FC kutoka Tanzania, Jumamosi hii inamenyana na Medeama FC ya Ghana katika mchuano wake wa tatu kuwania taji la Shirikisho.

Mechi hii inachezwa kuanzia saa 10 kamili saa za Afrika Mashariki katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Huu ni mchuano muhimu kwa Yanga FC ambayo imefungwa mechi mbili za kwanza katika michuano hii.

Wawakilishi hawa wa Tanzania katika mchuano wa kwanza walifungwa ugenini na MO Bejaia ya Algeria bao 1 kwa 0 lakini baadaye ikafungwa pia bao 1 kwa 0 na TP Mazembe mwezi uliopita jijini Dar es salaam.

Mchuano wa leo ni muhimu kwa Yanga FC ambayo ni ya mwisho katika kundi lake la A bila ya alama yoyote, nyuma ya Medeama, MO Bejaia na TP Mazembe.

Kesho Jumapili, viongozi wa kundi hili TP Mazembe watakuwa ugenini kupambana na MO Bejaia ya Algeria.

FUS Rabat ya Morocco wakiwa ugenini waliwafunga na Kawkab Marrakech mabao 3 kwa 1 na sasa inaongoza kundi B kwa alama 7 mbele ya Kawkab Marrakech ambayo ina alama 6.

Mchuano mwingine ni kati ya Etoile du Sahel ya Tunisia watakaopambana na Al-Ahli Tripoli ya Libya.

ZESCO United, itakuwa mwenyeji wa ASEC Mimosas ya Cote D'voire katika mchuano wa kundi A kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika.

Wawakilishi hawa wa Zambia wanakwenda katika mchuano huu wakiwa katika nafasi ya 3 kwa alama 3, baada ya kushinda mchezo mmoja dhidi ya Al-Ahly ya Misri na kufungwa na Wydad Casablanca.

Mchuano mwingine wa leo ni kati ya Al Ahly ya Misri dhidi ya Wydad Casablanca.

Kundi hili linaongozwa na Wydad Casblanca kwa alama 6, ikifuatwa na ASEC Mimosas ambayo ina alama 3 sawa na ZESCO United lakini Al-Ahly ni ya mwisho bila ua alama yoyote.

Kundi la B, Zamalek ya Misri itachuana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika kundi hilo ambalo limesalia na vlabu vitatu baada ya ES Setif kuondolewa katika michuano hii.

Mamelodi Sundowns wanaongoza kundi hili kwa alama 3, huku ikifuatwa na Zamalek ambayo pia ina alama 3.

Enyimba ya Nigeria ambao imecheza michuano mwili kundi hili, haijashinda mchuano wowote huku ikitarajiwa kucheza mechi yake ya tatu dhidi ya Zamalek mwezi ujao.