CAF

Sundowns, TP Mazembe zaendelea kung'ara klabu bingwa na kombe la shirikisho Afrika

cafonline

Klabu ya Afrika Kusini, Mamelodi Sundown imefanikiwa kupata ushindi muhimu kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika, baada ya kuifunga klabu ya Zamalek kutoka Misri, kwa jumla ya mabao 2-1 jijini Cairo.

Matangazo ya kibiashara

Kwa ushindi huo, Sundowns sasa imejihakikishia nafasi ya kutinga kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika huku ikiwa imesalia na michezo miwili kibindoni.

Mamelodi walifika kwenye hatua hii ya makundi baada ya kutupwa nje kwa klabu ya DRC, Vita Club, baada ya kumchezesha mchezaji aliyekuwa anatumikia adhabu.

Kwenye mechi nyingine za mwishoni mwa juma, Zesco United waliwafunga ASEC Mimosas ya Ivory Coast huku Al Ahly wakitoka sare na Wydad Casblanca ya Moroko.

Magoli ya Mamelodi yamefungwa na Tiyani Mabunda na Khama Billiat.

Timu hiyo sasa inaongoza kwenye kundi lake kwa alama 6, mbele ya Zamalek yenye alama 3 na Enyimba inayoshika mkia kwenye kundi hilo ikiwa haijapata alama yoyote.

Katika michezo ya kombe la shirikisho barani Afrika, nayo ilishuhudiwa ikitimua vumbi mwishoni mwa juma, ambapo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, Yanga ya Tanzania, waliwakaribisha Medeama ya Ghana, ambapo mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

TP Mazembe ya DRC yenyewe ilisafiri hadi nchini Algeriam ambako ilikuwa na kibarua dhidi ya Mouloudia Bejaia, kwenye mchezo ambao ulishuhudia timu hizo zikitoshana nguvu ya bila kufungana.

Kwa matokoe haya ya michezo ya kundi A, TP Mazembe wanaongoza wakiwa na alama 7, wakifuatiwa na Mo Bejaia yenye alama 5, Medeama yenye alama 2 na Yanga ya Tanzania inayoshika mkia kwa alama 1.

Mechi nyingine za kundi B zilichezwa juma lililopita, ambapo klabu ya Kawkab Marrakech wakiwa uwanja wa nyumbani walilala mbele ya ndugu zao, FUS Rabat, kwa kukubali kichapo cha mabao 3-1.

Etoile du Sahel wao walirekodi ushindi wao wa kwanza kwenye hatua hii, baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya klabu ya Al Ahly Tripoli ya Libya.