OLIMPIKI-BRAZIL 2016

Rais Kenyatta awataka wanamichezo wanaoenda Rio, kuiletea heshima nchi

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akikabidhi bendera ya Kenya kwa wanariadha na wanamichezo wa nchi hiyo wanaoenda kushiriki michezi ya Olimpiki ya Rio, 22 Julai 2016
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akikabidhi bendera ya Kenya kwa wanariadha na wanamichezo wa nchi hiyo wanaoenda kushiriki michezi ya Olimpiki ya Rio, 22 Julai 2016 Kenya Government

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amewakabidhi bendera ya taifa wanamichezo 185 watakaoiwakilisha nchi hiyo katika michezo ya Olimpiki itakayoanza nchini Brazil kuanzia tarehe 5 mwezi ujao nchini Brazil.

Matangazo ya kibiashara

Kenyatta amewaambia wanamichezo hao wakiwemo wanariadha, kuwa wahakikishe wanarejea nyumbani na medali nyingi za dhahabu na kuonesha dunia kuwa wanaweza kuwa mabingwa bila kutumia dawa zozote za kuongeza nguvu mwilini.

“Nendeni mtuwakilishe vizuri, waonesheni kuwa mnaweza kushinda kwa njia safi, wakenya wote watakuwa wanawafuata kwa makini,” alisema rais Kenyatta.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, akiteta jambo na mmoja wa wanariadha wanaoenda kushiriki michezo ya Rio, Brazil, 2016
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, akiteta jambo na mmoja wa wanariadha wanaoenda kushiriki michezo ya Rio, Brazil, 2016 Kenya Government

Amewata wanariadha kama Ezekiel Kemboi, bingwa wa dunia mbio za Mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa upande wa wanaume na bingwa mtetezi wa Mita 800 David Rudisha kuhakikisha kuwa wanatetea mataji yao katika michuano hii.

Waziri wa Michezo Hassan Wario amesema kuelekea katika michezo hii, vipimo zaidi ya 400 vimefanywa kwa wanariadha wa nchi hiyo kubainisha kuwa hawajatumia dawa hizo.

Rais Kenyatta akifurahia jambo na wanamichezo wa Kenya wanaoelekea Rio, Brazil
Rais Kenyatta akifurahia jambo na wanamichezo wa Kenya wanaoelekea Rio, Brazil Kenya Government

Mbali na riadha, Kenya itashiriki katika michezo mingine kama raga, bondia, Judo, uongoleaji na ule wa urushaji wa mkuki.

Kundi la kwanza la wachezaji wa Kenya linaondoka kesho kwenda jijini Rio de janeiro.