OLIMPIKI-BRAZIL 2016

Fahamu historia fupi ya michezo ya Olimpiki

Nembo ya michezo ya Olimpiki
Nembo ya michezo ya Olimpiki REUTERS/Ricardo Moraes

Historia inaonesha kuwa Michezo ya Olimpiki ilianza zaidi ya miaka 3,000 iliyopita katika mji wa Olympia, Kusini Magharibi mwa nchi ya Ugiriki.

Matangazo ya kibiashara

Madhumuni ya michezo hii ilikuwa ni tamasha la kidini, kumtukuza Zeus ambaye alikuwa ni Mfalme wa miungu nchini humo na ilikuwa inafanyika kila baada ya miaka minne.

Wakati huo, watu wote nchini Ugiriki walishiriki kwa pamoja katika tamasha hilo mbele ya Mfalme huyo.

Lakini mwaka 1896, michezo ya kisasa ya Olimpiki yalifanyika kwa mara ya kwanza jijini Athens.

Mwaka huo, wanamichezo 280 wote wakiwa wanaume kutoka mataifa 13 walishiriki katika michezo 43.

Michezo ambayo ilishindaniwa wakati huo ni pamoja na kukimbiza baiskeli, Tennis na unyanyuaji wa vyuma miongoni mwa michezo nyingine.

Vita vya dunia vilisababisha michezo hiyo kutofanyika mwaka 1916, 1940 na 1944, huku nchi nyingi zikijiondoa kushiriki katika michezo ya mwaka 1980 na 1984 kwa sababu ya vita baridi vya dunia.

Hata hivyo, ilipofika mwaka 1994 michezo hii iligawanywa mara mbili ile ya msimu wa joto na baridi, na tofauti ya michezo hiyo ilikuwa ni miaka 2.

Michezo hii inasimamiwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ambayo ina jukumu la kuandaa michezo hii, ikiwa ni pamoja na kutafuta mji wa kuandaa michezo hiyo lakini pia kutafuta fedha za kuifadhili.

Ishara ya michezo hii ni bendera na mwenge.

Michezo hii pia hutoa nafasi kwa nchi na mji unaoandaa michezo ya Olimpiki kujitangaza kwa dunia na kuonesha mambo yake kwa maelfu ya wageni wanaohudhuria michezo hii.

Ni michezo ambayo pia katika historia yake imekuwa ikitawaliwa na ususiaji, wanamichezo kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini ili kushinda, ufisadi na hata shambulizi la kigaidi.

Mwaka 1972 wakati michezo hii ilipofanyika mjini Munich nchini Ujerumani, wakati huo ikiwa ni Ujerumani Magharibi, wanamichezo na maafisa wa Israel 11 walitekwa na kuuawa na kundi la kigaidi kutoka Palestina.

Mshindi wa kwanza katika michezo mbalimbali hutuzwa medali ya dhahabu, mshindi wa pili medali ya fedha na mshindi wa tatu medali ya shaba.

Medali za michezo ya Olimpiki, dhahabu, fedha na shaba
Medali za michezo ya Olimpiki, dhahabu, fedha na shaba

Wanamichezo walemavu pia wamepata nafasi ya kushiriki katika michezo hii tangu mwaka 1960, lengo lilikuwa ni kuwapa nafasi wanajeshi waliokuwa wamejeruhiwa na kuwa walemavu baada ya vita vya dunia kuonesha vipaji vyao katika michezo mbalimbali.

Michezo ya walemavu hufanyika kipindi cha joto kila mwaka wakati wa michezo ya kawaida ya Olimpiki ya majira hayo.

Oscar Pistorius mwanariadha mlemavu
Oscar Pistorius mwanariadha mlemavu npr

Bara la Afrika halijawahi kupata fursa ya kuwa mwenyeji wa michezo hii.

Marekani ndio nchi peke duniani ambayo imeandaa michezo hii mara nyingi ikiwa ni mara 8.

Kipindi cha joto Marekani imekuwa mwenyeji mwaka 1904,1932,1984 na 1996 huku yale ya kipindi cha baridi yakifanyika mara nne pia mwaka 1932,1960,1980 na 2002.

Miji ambayo imekuwa maarufu kuandaa michezo hii ni Los Angeles na Lake Placid.

Ufaransa nayo imeandaa mara 5, Japan mara 4 huku Uingereza, Canada , Italia na Ujerumani ikiandaa mara 3.

Msemo wa michezo hii ni kuwa, ukifuzu katika michezo hii siku zote utakuwa mwanaolimpiki.