OLIMPIKI-BRAZIL 2016

Fahamu mwafrika wa kwanza kushinda medali ya dhahabu michezo ya Olimpiki

Abebe Bikila aliposhinda medali ya dhahabu mbio za Marathon mwaka 1960
Abebe Bikila aliposhinda medali ya dhahabu mbio za Marathon mwaka 1960

Michezo ya Olimpiki inaanza Ijumaa ijayo jijini Rio rio de janeiro nchini Brazil.

Matangazo ya kibiashara

Haya yatakuwa ni mashindano ya msimu wa joto na tayari maelfu ya wanamichezo kutoka mataifa mbalimbali duniani wamewasili nchini Brazil .

Wakati kama huu, wanariadha duniani hukumbuka historia yao katika michezo hii.

Ukizungumzia mbio za masafa marefu kama Marathon,  Mita 10,000 na 5,000 lazima utawataja wanariadha kutoka Afrika Mashariki hasa nchini Kenya na Ethiopia.

Mwaka 1960 wakati michezo hii ilifanyika mjini Rome nchini Italia, Abebe Bikila kutoka Ethiopia alikuwa ni mwafrika wa kwanza kunyakua medali ya dhahabu katika michezo hii.

Alishinda mbio za Marathon kwa upande wa wanaume kwa kutumia muda wa saa 2 dakika 15 na sekunde 16, mbio ambazo alikimbia bila ya kuvaa viatu .

Aliporudi jijini Addis Ababa, alipokelewa na maelfu ya raia wa nchi hiyo na uwanja wa michezo kutajwa kwa jina lake. Uwanja wa Abebe Bikila.

Miaka minne baadaye mwaka 1964 jijini Tokyo nchini Japan, Bikila alitetea taji lake kwa kuweka muda bora wa saa 2 dakika 12 na sekunde 11.

Kipchoge Keino ni mwanariadha mwingine za amani lakini kutoka nchini Kenya ambaye pia alishinda medali mbili za dhahabu katika michezo hii.

Mwaka 1968 wakati michezo hii ilipofanyika nchini Mexico, alipata dhahabu katika mbio za Mita 1500, huku akishinda dhahabu pia mwaka 1972 katika mbio za Mita 3000 wakati michezo hiyo ilipofanyika mjini Munich nchini Ujerumani.

Hao ni wanariadha kutoka Afrika Mashariki walioweka historia katika michezo hii.

Ushindani huo unatarajiwa kushuhudiwa katika michezo ya mwaka huu.