OLIMPIKI-BRAZIL 2016

Sudan Kusini kushiriki michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza

Sudan Kusini inaweka historia kwa kushiriki kwa mara ya kwanza katika michezo ya Olimpiki itakayoanza Ijumaa ijayo nchini Brazil.

Santino Kenti mwanariadha wa Sudan Kusini akifanya mazoezi
Santino Kenti mwanariadha wa Sudan Kusini akifanya mazoezi wordpress.com
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inakuja baada ya nchi hiyo iliyopata uhuru wake mwaka 2011 kuwa mwanachama wa 206 wa Kamati ya Kimataifa ya michezo ya Olimpiki IOC mwezi Agosti mwaka uliopita.

Kabla ya kujiunga na IOC kabla ya kuwa huru, nchi hii imekuwa ikishiriki katika michezo hii tangu mwaka 1960 ilipokuwa nchi moja ya Sudan.

Michezo ya mwaka huu, Sudan Kusini itawakilishwa na wanariadha wawili Santino Kenti atakayeshiriki katika mbio za Mita 1500 kwa upande wa wanaume.

Margret Rumat Hassan naye atashiriki katika mbio fupi za Mita 200 na 400 kwa upande wa wanawake.

Kamati ya IOC imeiruhusu nchi hiyo kushiriki katika michezo ya riadha, kikapu, soka, mchezo wa mkono, judo, Tenis ya mezani na Taekwondo.