USAJILI-MANCITY

Man City yakamilisha rekodi ya usajili wa beki John Stones kutoka Everton

Mchezaji wa zamani wa Everton ambaye sasa amejiunga na klabu ya Manchester City
Mchezaji wa zamani wa Everton ambaye sasa amejiunga na klabu ya Manchester City Reuters / Lee Smith Livepic

Hatimaye klabu ya Manchester City imefanikiwa kumsajili beki wa kati kutoka klabu ya Everton, John Stone, kwa dau la pauni za Uingereza milioni 47.5, dau ambalo linamfanya kuwa beki wa pili ghali zaidi duniani baada ya aliyekuwa beki wa kati wa Manchester United, Rio Ferdinand.

Matangazo ya kibiashara

Mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 22 anayechezea pia timu ya taifa ya Uingereza, amesaini mkataba wa miaka 6 kuitumikia klabu hiyo ya Manchester, na anakuwa mchezaji wa nane kusajiliwa na kocha Pep Guardiola.

Awali Stones alikuwa ameorodheshwa kwenye kikosi cha wachezaji wa Manchester City watakaoichezea timu hiyo kwenye michuano ya klabu bingwa Ulaya, ambapo jina lake lilionekana kwenye mtandao wa uefa hata kabla ya usajili wake kukamilika.

Akizungumza mara baada ya kumaliza taratibu za usajili wake, Stones amesema "Sasa suala hili limemalizika na natarajia mazuri katika maisha yangu ya soka," alisema Stones.

Mchezaji huyu ameongeza kuwa kutokana na yale anayoyaona kwenye klabu ya Manchester City, ni wazi kuwa inatarajia makubwa kwenye ukanda wa Ulaya na kwamba haikuwa shida sana kwake kukubali uhamisho huo.