RIO OLIMPIKI 2016

RIO OLIMPIKI 2016: Muogeleaji Efimova aendelea kukosolewa

Muogeleaji raia wa Marekani, Michael Phelps ambaye ameshinda medali yake ya 19 ya dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki ya Rio, Brazil
Muogeleaji raia wa Marekani, Michael Phelps ambaye ameshinda medali yake ya 19 ya dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki ya Rio, Brazil REUTERS/Dominic Ebenbichler

Muogeleaji Michael Phelps raia wa Marekani amesema, inaumiza moyo kuona wanamichezo waliowahi kufungiwa kutokana na kutumia dawa za kusisimua misuli, wanaruhusiwa kushiriki kwenye michezo ya Olimpiki inayofanyika mjini Rio, Brazil. Phelps mwenye umri wa miaka 31, alirejea kwenye  michezo ya mwaka huu baada ya awali kutangaza kustaafu na sasa anashiriki michezo ya tano ya Olimpiki, ambapo tayari ameshajipatia medali yake ya 19 ya dhahabu.

Matangazo ya kibiashara

Phelps ametoa matamshi haya kukashifu wachezaji wanaotumia dawa za kusisimua misuli, baada ya mchezaji wa Urusi aliyefungiwa mara mbili, Yulia Efimova, kushinda medali ya fedha kwenye mchezo wa kuogelea upande wa wanawake mita 100.

Phelps amesema "ni huzuni leo hii tunapozungumzia michezo kwa ujumla, sio tu kuogelea, kuna watu ambao majibu yao yamekuwa chanya kwa kutumia dawa za kusisimua misuli na wanaruhusiwa kurudi kwenye michezo tena zaidi ya mara moja."

"Naamini michezo inabidi kuwa safi na inabidi kuwa michezo yenye usawa uwanjani, na nafikiri ni huzuni sana kwamba leo hii tunao watu wanaoshiriki michezo huku vipimo vyao vikiwa chanya na sio mara moja tu lakini mara mbili na bado wamepewa nafasi ya kushiriki." alisema Phelps.

"Inaumiza moyo wangu na natamani kuona mtu mmoja anafanya kitu chochote kuhusu hili."

Mchezaji wa Urusi, Efimova alifungiwa miezi 16 mwaka 2013 baada ya vipimo vya damu yake kuonesha kuwa na chembechembe za Steroid ambazo zinakatazwa kwenye mwili.

Muogeleaji wa Urusi, Yulia Efimova ambaye alifungiwa kwa zaidi ya mara mbili lakini ameshiriki michezo ya Olimpiki ya Rio, 2016
Muogeleaji wa Urusi, Yulia Efimova ambaye alifungiwa kwa zaidi ya mara mbili lakini ameshiriki michezo ya Olimpiki ya Rio, 2016 REUTERS/Dominic Ebenbichler

Na mapema mwaka huu alipewa kifungo cha muda baada ya vipimo kuonesha kwa mara nyingine kuwa na chembechembe za meldonium, lakini shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani Fina likaondoa adhabu hiyo baada ya kupata ushauri kutoka kwa shirika la kupambana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli mchezoni Wada.

Kamati ya kimataifa ya Olimpiki ilitoa uamuzi kuwa, kwenye michezo ya mwaka huu, hakuna mchezaji atakayeruhusiwa kushiriki ikiwa alipatikana na hatia ya kutumia dawa za kusismua misuli, lakini Efimova aliruhusiwa kushiriki kufuatia rufaa yake aliyokata kwenye mahakama ya kimataifa ya michezo Cas.

Muogeleaji mwenza wa Phelps kwa upande wa wanawake, Lily King ambaye alimshinda Efimova kwenye mita 100 mtindo wa kurudi nyuma, alikosa pia muogeleaji huyo kuruhusiwa kushiriki michezo ya mwaka huu.

Efimova mwenyewe ambaye wakati wote wa ushiriki wa michezo ya mwaka huu amekuwa akizomewa na mashabiki, amesema kuwa "ni huzuni na inakasirisha. Binafsi nawajua wanamichezo wengi tu ambao ni wasafi, lakini wamezuiwa kushiriki kwasababu ya Urusi.

"Kila kitu kilichotokea kwangu mimi ni maajabu. Nilifanya makosa na nikafungiwa kwa miezi 6. Mara ya pili haikuwa kosa langu." Alisema Efimova.