RIO OLIMPIKI

Bolt kukimbia mita 200, Kemboi abadili uamuzi kustaafu riadha, Brazil vs Ujerumani fainali

Mwanariadha wa Jamaica, Usain Bolt ambaye atashiriki fainali ya mbio za mita 200 jijini Rio, Brazil
Mwanariadha wa Jamaica, Usain Bolt ambaye atashiriki fainali ya mbio za mita 200 jijini Rio, Brazil REUTERS/Dylan Martinez

Katika michezo ya Olimpiki inayoendelea jijini Rio De Jeneiro, Brazil, mfukuza upepo Usain Bolt raia wa Jamaica amefanikiwa kushinda hatua ya nusu fainali ya mbio za mita 200 na kuingia hatua ya fainali, akitarajiwa kuweka rekodi ya kutwaa medali ya tatu mfululizo kwenye michezo ya Olimpiki ya dunia. 

Matangazo ya kibiashara

Wanariadha wengine wa Jamaica Yohan Blake na Mmarekani Justin Gatlin wao walishindwa kufuzu kuingia hatua ya fainali kwenye mbio za mita 200.

Juma hili tayari Bolt ameshajinyakulia medali ya dhahabu kwenye mita 100, na sasa anasubiriwa kushiriki kwenye mita 200 na kisha mita 400 kupokezana kijiti akiwakilisha timu ya Jamaica.

Katika hatua nyingine mwanariadha wa Kenya, Ezekiel Kemboi, ambaye ni bingwa mara mbili kwenye michezo ya Olimpiki mita elfu 3000 kuruka viunzi na maji, amebadili uamuzi wake wa kustaafu riadha mwaka huu na kuahidi kurejea kwanguvu kwenye mashindano ya dunia ya riadha jijini London mwakani.

REUTERS/Dylan Martinez

Kemboi ambeye ameshinda mbio za dunia mita elfu 3, mara tano! Amesema angestaafu riadha ikiwa angenyakua medali ya dhahabu nchini Brazili baada ya kuondolewa kutokana na kuingia vibaya kwenye mstari wake wa kukimbilia na hivyo kukosa medali.

Kwa upande wa wanawake, Mjamaica Elaine Thompson ameshinda mbio za mita 200 na kukamilisha medali zake mbili kwenye michezo ya Olimpiki, ambapo pia aliweka kibindoni medali ya dhahabu katika mbio za mita 100 upande wa wanawake.

Katika mbio za mita 400 kupokezana kijiti, wanariadha wa Ujerumani, Nigeria na TriniDad and Tobago wamefuzu kwenye hatua ya fainali ya mbio hizo huku Marekani na Uholanzi wakishindwa kufuzu.

Katika kabumbu, timu ya taifa ya Brazil imefanikiwa kutinga kwenye hatua ya fainali kusaka medali ya dhahabu kwa kuweka historia pia ya kufunga bao la mapema zaidi katika michezo ya Olimpiki, lililofungwa Sekunde ya 14 tu mchezo na nahodha wake Neymar.

Brazil iliisambaratisha Honduras kwa mabao 3-0 huku Ujerumani wao wakifuzu hatua ya fainali baada ya kuwafunga wawakilishik wa Afrika timu ya taifa ya Nigeria kwa mabao 2-0.

Kwa matokeo hayo, Nigeria itacheza kutafuta mshindi wa tatu dhidi Honduras kuwania medali ya shaba.

Wachezaji wa Uingereza wakisherekea ushindi.
Wachezaji wa Uingereza wakisherekea ushindi. REUTERS/Vasily Fedosenko

Katika mchezo wa magongo ama Hockey, timu ya taifa ya wanawake ya Uingereza imefanikiwa kutinga hatua ya fainali kwa mara ya kwanza baada ya kuwafunga New Zealand kwa mabao 3-0, na sasa watakutaka kwenye fainali siku ya Ijumaa ambapo watacheza dhidi ya Uholanzi.

Katika mchezo wa kukata upepo kwenye maji, waingereza Hannah Mills na Saskai Clark wanasubiri kupewa ubingwa wa wanawake kwenye mita 470 baada ya mashindano yao kuahirishwa huku kwa upande wa wanaume mashindano yao yakifutwa kutokana na upepo kutokuwepo wa kutosha.

Marekani bado inaongoza kwenye orodha ya nchi zilizojinyakulia medali nyingi zaidi za dhahabu, huku Uingereza pamoja na China zikifungana kwa medali za dhahabu ambapo zinadhahabu 19 kila mmoja.