OLIMPIKI-BRAZIL 2016-RIADHA

Kemboi apokonywa medali ya shaba

Mwanariadha wa Kenya Ezekiel Kemboi
Mwanariadha wa Kenya Ezekiel Kemboi REUTERS/Dylan Martinez

Ezekiel Kemboi, amepokonywa medali ya shaba aliyoishindia nchi yake ya Kenya katika mbio za Mita 3000 kuruka viunzi na maji katika michezo ya Olimpiki nchini Brazil siku ya Jumatano.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo ilichukuliwa na Shirikisho la riadha duniani IAAF, baada ya kubainika kuwa alikimbilia nje ya eneo maalum kwa mujibu wa kanuni za riadha baada ya Ufaransa kulalamika.

Baada ya uamuzi huo Mfaransa Mahiedine Mekhissi aliyemaliza nafasi ya nne, alitunukiwa medali hiyo ya shaba.

Kemboi mwenye umri wa miaka 34 na bingwa mara mbili katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2004 na 2012 amehuzunishwa na hatua hiyo baada ya kutangaza kuwa anastaafu riadha.

Hata hivyo, Kenya iliendeleza rekodi yake ya kunyakua medali ya dhahabu katika mbio hizi baada ya Conseslus Kipruto kuibuka bingwa.