RIO OLIMPIKI 2016

Mkenya Boniface Mucheru aweka historia Rio, Brazil

Mwanariadha wa Kenya, Boniface Mucheru, ambaye ameweka historia kwa nchi yake kwa kutwaa medali ya fedha kwenye michezo ya Olimpiki, 18 Agosti, 2016
Mwanariadha wa Kenya, Boniface Mucheru, ambaye ameweka historia kwa nchi yake kwa kutwaa medali ya fedha kwenye michezo ya Olimpiki, 18 Agosti, 2016 REUTERS/Alessandro Bianchi

Bingwa wa Afrika katika mbio za mita 400 kuruka viunzi, Boniface Mucheru, Alhamisi ya Agosti 18, 2016 ameweka historia kwenye michezo ya Olimpiki ya Rio na kuwa Mkenya wa kwanza kushinda medali ya fedha kwenye mbio hizo.

Matangazo ya kibiashara

Katika mbio hizom sio tu Mucheru ameweka rekodi binafsi ya muda wa sekunde 47.78, pia amevunja rekodi ya kitaifa ya sekunde 47.79 ambayo ilikuwa inashikiliwa na Nicholas Bett wakatik akishinda taji la mashindano ya dunia ya Beijing mwaka uliopita.

Mucheru mwenye umri wa miaka 24, alianza mbio hizo akiwa nyuma na kujaribu kuwapiku wapinzani wake, lakini akajikuta juhudi zake zikigonga mwamba mbele ya Mmarekani Kerron Clement ambaye alishinda medali ya fedha kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008, kwa kumaliza kwa sekunde 47.73, huku mwanariadha wa Uturuki Yasmani Copello akishinda medali ya shaba kwa kumaliza kwa sekunde 47.92.

Mucheru ambaye aliingia kwenye mbio hizo akiwa na rekodi binafsi ya muda wa sekunde 48.89, anakuwa Mkenya wa tatu kushinda medali kwenye michezo ya Olimpiki kuruka viunzi baada ya Julius Sang ambaye alishinda medali ya shaba kwenye mbio za mita 400 wakati wa michezo ya Olimpiki ya mwaka 1972 iliyofanyika Munich Ujerumani na Samson Kitur aliyeshinda medali ya shaba pia kwenye mita 400 mwaka 1992 mjini Barcelona, Hispania.

Mucheru alishinda medali ya shaba kwenye mbio za mita 400 na 4x400 mwaka 2010 wakati wa mashindano ya Africa Championship kabla ya kushinda medali nyingine ya shaba katika mita 400 na 4x400 mwaka 2014 kwenye michezo kama hiyo.

Mwanariadha huyu alimaliza kwenye nafasi ya 35 wakati wa michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012 na kumaliza kwenye nafasi ya 15 kwenye mbizo za mita 4x400 mwaka 2014 wakati wa mashindano ya dunia kabla ya kushinda kwenye mashindano ya jumuiya ya Madola mwaka 2014 ambapo alikimbia mita 400.

Alishika nafasi ya 5 kwenye mbio za mita 400 wakati wa mashindano ya dunia mwaka 2015 kabla ya kushinda medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Afrika yaliyofanyika mwaka huu.