WCQF 2018-ULAYA

Uingereza, Ujerumani zaanza vema mechi za kufuzu kuelekea kombe la dunia 2018

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uingereza, Adam Lallana akiwa anashangilia kwa kujifunika uso na jezi yake wakati alipoiandikia timu yake goli la ushindi dhidi ya Slovakia, September 4, 2016
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uingereza, Adam Lallana akiwa anashangilia kwa kujifunika uso na jezi yake wakati alipoiandikia timu yake goli la ushindi dhidi ya Slovakia, September 4, 2016 Reuters / Carl Recine Livepic

Mechi za kuwania kufuzu kucheza kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi, zimeendelea kwenye bara la Ulaya, ambapo mwishoni mwa juma mataifa kadhaa yalikuwa uwanjani kutupa karata zao za awali za kutafuta kufuzu kwenda Urusi.

Matangazo ya kibiashara

Mechi za mwishoni mwa juma na zile ambazo zitapigwa kuanzia juma hili, ni muhimu kwa mataifa hayo ya Ulaya, ambayo kila timu inahitaji ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuhakikisha zinafuzu kwenda Urusi.

Timu ya taifa ya Uingereza ikiwa chini ya Kocha mpya, Sam Alardayce, ilifanikiwa kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Slovakia, ikiwalazimu kusubiri hadi kwenye dakika za lala salama kupata bao muhimu na la ushindi kupitia kwa mchezaji wake Adam Lallana.

Mchezo huo ulikuwa ni wa kwanza wa Alardayce, ambapo naye anatengeneza historia ya makocha wengine 8 waliopita kuinoa timu hiyo, ambapo walishinda kwenye mechi zao za kwanza baada ya kuchukua kibarua.

Baada ya mchezo huo, Alardayce aliwakosoa washambuliaji wake kwa kushindwa kupachika mabao, huku akikosoa mtindo aliosema wa kupaki basi uliotumiwa na timu ya Slovakia kulinda lango lao.

Kwenye mechi nyingine, San Marino walikuwa nyumbani kuwakaribisha Azerbaijan katika mchezo ambao ulishuhudia, Azerbaijan ikiibuka na ushindi wa bao 1-0, huku Mata wakiwa nyumbani, walikubali kichapo cha mabao 5-1 dhidi ya Scotland.

Romania wakiwa nyumbani, wao walilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Montenegro, huku Norway wakiwa nyumbani waliwakaribisha timu ya taifa ya Ujerumani, kwenye mchezo ambao, Ujerumani iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Timu ya taifa ya Jamhuri ya Czech yenyewe ilikuwa nyumbani kucheza na Ireland Kaskazini, katika mchezo ambao ulishuhudia timu hizo, zikitoshana nguvu kwa kutofungana, huku Lithuania wakiwa nyumbani, nao walijikuta wakilazimishwa sare ya mabao 2-2 wakiwa nyumbani dhidi ya Slovenia.

Kazakhstan wakiwa nyumbani walipepetana na timu ya taifa ya Poland, katika mchezo ambao na wenyewe ulimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu, kwa kufungana mabao 2-2.

Mechi nyingine, Denmark wakiwa nyumbani walifanikiwa kuutumia vema uwanja wake wa nyumbani, baada ya kufanikiwa kuchomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya taifa ya Armenia, kwenye mchezo uliokuwa wa kuvutia kwa muda wote wa dakika tisini.