SOKA-UINGEREZA

Allardyce asema ajutia matamshi yake yaliyomsababisha kuacha kazi

Aliyekuwa kocha wa Uingereza  Sam Allardyce
Aliyekuwa kocha wa Uingereza Sam Allardyce REUTERS/Carl Recine/File Photo

Sam Allardyce amesema amesikitika sana kuacha kazi yake kama kocha wa timu ya taifa ya soka ya Uingereza, baada ya kuwa katika wadhifa huo kwa siku 67.

Matangazo ya kibiashara

Allardayce alilazimika kusalimu amri baada ya Gazeti la Telegram kuripoti kuwa alihusika katika njama za kugeuza taratibu za kuwasajili wachezaji kinyume na utaratibu wa Shirikisho la soka nchini humo na kumtumia mtu wa tatu katika zoezi hilo.

Kocha huyo ameomba msamaha na kusema kuwa matamshi yaliyosika katika mkanda ulionaswa kisiri umeleta aibu kubwa na hivyo hawezi kuendelea kuwa kocha wa Uingereza.

Shirikisho la soka nchini humo limesema limesikitishwa na matamshi ya kocha huyo na hivyo, amekubali kuacha kazi baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa soka.

Gareth Southgate ameteuliwa kwa muda kuifunza timu kwa mechi nne zijazo, wakati huu kocha mpya akitafutwa kuziba pengo la Allardayce.

Inadaiwa kuwa mwaka 2014, kocha huyo akiwa na wakala wake na mshauri wake wa kifedha, alifanikisha usajili wa mchezaji Enner Valencia raia wa Ecuador kuichezea klabu ya West Ham  nchini Uingereza kutoka klabu ya Pachuca kutoka Mexico kwa kima cha Pauni Milioni 12.

Shirikisho la soka nchini Uingereza lilipiga marufuku mchakato wa wachezaji kusajiliwa kupitia mtu wa tatu mwaka 2008.