CAF U17

Timu za vijana U17 zitakazocheza kombe la mataifa ya Afrika mwakani zajulikana

Nembo ya shirikisho la soka Afrika, CAF
Nembo ya shirikisho la soka Afrika, CAF

Timu zitakazocheza fainali ya kombe la mataifa ya Afrika, iliyopangwa kufanyika nchini Madagascar mwakani kwa upande wa vijana chini ya umri wa miaka 17, hatimaye zimejulikana mara baada ya michezo ya mwishoni mwa juma.

Matangazo ya kibiashara

Mechi za mwishoni mwa juma zilikuwa ni zakukamilisha ratiba ya hatua ya kufuzu kucheza fainali hizo, baada ya mechi za kwanza zilizochezwa takribani majuma mawili yaliyopita.

Hapo wawakilishi pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki waliokuwa wamesalia kwenye hatua ya kufuzu, timu ya taifa ya vijana wa Tanzania, ndoto zake kufuzu kwa mara ya kwanza zilizimika nchini Congo Brazaville, baada ya kuondolewa kwa mikwaju ya penalt.

Kwenye mchezo wa awali uliofanyika jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, timu ya vijana ya Tanzania ilipata ushindi wa mabao 3-2 na ilihitaji sare tu nchini Congo ili ifuzu, lakini ilijikuta ikifungwa kwa bao 1-0 na kulazimika mchezo wao kuamuliwa kwa penalt, ambapo Congo ilipata penalt 8-7.

Congo imefuzu kucheza fainali za mwakani nchini Madagascar.

Kwenye mechi nyingine, Cameroon wakiwa nyumbani walicheza na Sudan katika mchezo ambao ulishuhudia, Cameroon wakiibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1, huku kwenye mchezo wa awali, Sudan walishinda kwa mabao 4-2, lakini sasa wametolewa kwa tofauti ya magoli 7-5.

Cameroon imefuzu kucheza fainali hizo mwakani.

Guinea wao walilazimishwa sare ya mabao 2-2 na timu ya vijana ya Senegal, kwenye mchezo ambao Senegal walihitaji ushindi, kwa kuwa kwenye mchezo wao wakiwa nyumbani walikubali kichapo cha bao 1-0.

Kwa matokeo haya, Guinea inafuzu kwa tofauti ya magoli 3-2.

Ethiopia, wenyeji wengine kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, walishindwa kukata tiketi ya kucheza fainali hizo licha ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali kwenye mchezo wa marudiano.

Kwenye mchezo wa awali Mali ikiwa nyumbani iliifunga Ethiopia kwa mabao 2-0, na hivyo imefuzu kwa tofauti ya mabao 4-2.

Timu ya vijana ya visiwa vya Comoros yenyewe ilikuwa nyumbani kucheza na Angola, katika mchezo ambao Angola waliibuka washindi kwa kuwafunga Comoros kwa mabao 2-0, huku kwenye mchezo wa awali Angola ikishinda kwa mabao 5-0.
Angola inafuzu kwa jumla ya mabao 7-0.

Gabon wao wakiwa nyumbani walilazimishwa sare ya mabao 3-3 na timu ya taifa ya vijana ya Niger, huku kwenye mchezo wa awali Niger wakiibuka na ushindi wa bao 1-0.

Niger yenyewe imefuzu kucheza fainali za mwakani kwa jumla ya mabao 4-3.

Ivory Coast wenyewe wakiwa nyumbani walilazimishwa sare ya bila kufungana na timu ya taifa ya vijana ya Ghana, huku katika mchezo wa awali uliofanyika jijini Accra, vijana wa Ghana waliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Ghana inafuzu kucheza fainali hizi kwa jumla ya mabao 3-1.

Timu zilizofuzu kucheza fainali hizi zinazotarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia April 2 hadi 16 mwaka 2017 nchini Madagascar, ni pamoja na Angola, Congo, Ghana, Niger, Mali, Guinea, na Cameron.