FIFA-GIANNI INFANTINO

Infantino: Zoezi la kuandaa fainali za kombe la dunia 2026 litakuwa huru na wazi

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu duniani Fifa, Gianni Infantino.
Rais wa shirikisho la mpira wa miguu duniani Fifa, Gianni Infantino. REUTERS/Arnd Wiegmann

Rais wa Fifa, Gianni Infantino, ameapa kuwa, mchakato wa zabuni ya kuandaa fainali za kombe la dunia za mwaka 2026 utakuwa huru na usiokuwa na mizengwe, kama ambavyo ilitawala wakati wa utoaji wa zabuni ya fainali za mwaka 2018 nchini Urusi na mwaka 2022 nchini Qatar. 

Matangazo ya kibiashara

Infantino amesema haya akijibu madai yaliyotolewa hivi karibuni na rais wa Marekani Barack Obama, kuwa mchakato wa maandalizi na utoaji wa zabuni kwa nchi zinazoandaa michezo ya Olimpiki na Kombe la Dunia umejaa rushwa.

“Siwezi kuzungumza kuhusu yaliyopita. Lakini naweza kukuahidi kuwa, lazima tuangalie kwa umakini sana maombi ya zabuni ya kuandaa kombe la dunia mwaka 2026 ili kujiridhisha kuwa mchakato mzima uko huru na wa haki,” alisema Infantino wakati akizungumza na shirika la habari la AFP.

Katika kipindi hiki ambacho shirikisho la mpira wa miguu duniani Fifa limekumbwa na kashfa za rushwa toka mwezi May 2015, kumekuwa na shinikizo la kurudiwa kwa kura kwenye utoaji wa zabuni kwa nchi ya Urusi na Qatar ambazo zitaandaa fainali za kombe la dunia ya mwaka 2018 na 2022.

Infantino amesema kuwa ni lazima kuhakikisha kuwa maandalizi ya utoaji wa zabuni kwaajili ya fainali za mwaka 2026, unazingatia utafiti na tathmini ya kiufundi kuhusu nchi zinazotaka kuandaa fainali hizo.

“Ni jukumu letu kufanya haya, kuhakikisha mchakato unakuwa wa wazi na uhuru, na kwamba wale wote wanaotaka kuandaa fainali hizo wanakuwa na muda wa kujiandaa kutoka sasa,” alisema Infantino.

Kwenye mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni, Rais Obama alitolea mfano namna ambavyo mji wa Chicago uliomba kuandaa michezo ya mwaka 2016 na kwamba wamejifunza kutoka Fifa kuwa mifumo inafanana na kwamba matokeo yake hutengenezwa.