SIERRA LEONE

Ligi kuu ya soka Sierra Leone kuanza tena baada ya kusimama kwa hofu ya ebola

Mchezaji wa timu ya taifa ya Sierra Leone akikabiliana na mchezaji wa timu ya taifa ya Ivory Coast.
Mchezaji wa timu ya taifa ya Sierra Leone akikabiliana na mchezaji wa timu ya taifa ya Ivory Coast. ISSOUF SANOGO / AFP

Shirikisho la mpira wa miguu nchini Sierra Leone linatarajia kuanza tena kuendesha ligi kuu ya soka nchini humo kwa mara ya kwanza toka taifa hilo likumbwe na mlipuko wa virusi vya ebola na kulazimisha ligi kusimama.

Matangazo ya kibiashara

Mara ya mwisho ligi hiyo kufanyika ilikuwa katikati ya msimu wa mwaka 2014 ambapo ilisimama baada ya kutangazwa kwa hali ya dharura kutokana na maradhi ya virusi vya ebola.

Nchi ya Sierra Leone ilitangazwa kuwa taifa huru dhidi ya maambukizi ya ebola na shirika la afya duniani WHO, mwezi Machi mwaka huu.

Michuano ya kwanza kufanyika nchini humo ilikuwa ni ile ya kombe la ligi, FA, ambapo ilimalizika Jumamosi ya wiki iliyopita, hali inayotoa mwanya wa kuanza tena kwa ligi kuu ya soka nchini humo baada ya kusimama kwa muda.

Lakini wakati klabu ya Johansen ikishinda taji lake la kwanza kwa kuifunga timu ya jeshi la Sierra Leone kwa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano wa fainali, michuano hiyo haikuwa na ushindani kutokana na kukosekana kwa baadhi ya timu 14 zinazoshiriki ligi hiyo.

Timu hizo zilisusia kushiriki mashindano hayo kwa kile wanachosema ni kuendelea kwa migogoro ndani ya chama cha soka nchini humo, SLFA, na kwamba huenda ligi ikaanza kwa kutumia mfumo ule ule ambao walikuwa wanaupinga.

Hata hivyo mkurugenzi wa SLFA, Sorie Ibrahim Sesay akizungumza na shirika la utangazaji la Uingereza, amesema ana matumaini kuwa ligi hiyo itaanza na timu hizo zitaacha mgomo wao.