ROONEY-TIMU YA TAIFA YA UINGEREZA

Rooney aachwa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa, akiri kuwa kwenye wakati mgumu

Nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza Wayne Rooney amesema kuwa, yuko katika wakati mgumu sana wa maisha yake ya soka, baada ya kuachwa nje kwenye kikosi cha timu yake kitakachoivaa timu ya taifa ya Slovenia kwenye mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza fainali za kombe la dunia nchini Urusi, mwaka 2018.

Nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza, Wayne Rooney ambaye ameachwa nje ya kikosi cha timu yake ya taifa.
Nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza, Wayne Rooney ambaye ameachwa nje ya kikosi cha timu yake ya taifa. Reuters/Gonzalo Fuentes
Matangazo ya kibiashara

Kocha wa mpito wa timu ya Uingereza, Gareth Southgate amesema kuwa, uamuzi aliouchukua wa kumuacha Wayne Rooney ni uamuzo wa kiufundi zaidi na hakuna uhusiano wowote na kile kinachomsibu kwa sasa mshambuliaji wake.

Rooney ambaye alizomewa na sehemu ya mashabiki kwenye dimba la Wimbley wakati timu yake ilipokuwa ikicheza na Malta na kuchomoza na ushindi wa mabao 2-1, hakuanza kwenye kikosi cha kwanza cha klabu yake ya Manchester United katika mechi 3 zilizopita.

Rooney mwenye umri wa miaka 30, amesema kuwa hajisikii vibaya kuanzia kwenye benchi.

Mshambuliaji huyo ambaye hivi karibuni amekuwa akichezeshwa kwenye nafasi ya kiungo, ataendelea kuwa nahodha wa timu hiyo, ambapo sasa kiungo wa Liverpool Jordan Henderson ataongoza kikosi hicho kwenye mchezo wa Jumanne ya October 11.

Rooney ambaye anashikilia rekodi ya ufungaji bora kwenye timu yake ya taifa na pia kama mchezaji aliyeichezea mara nyingi timu yake akiwa na mabao 53 katika michezo 117 aliyocheza, huku msimu huu akiwa amefunga goli moja pekee kwa timu yake ya taifa na klabu.

“Mchezo wangu sasa? Ndio, siwezi kukataa niko kwenye wakati mgumu sana.

Nimekuwa benchi kwenye michezo kadhaa ya klabu yangu ya Manchester United, lakini ni sehemu ya mpira wa miguu,” alisema Wayne Rooney.

“Lazima nifanye jitihada zaidi na wakati nikihitajika kwa klabu yangu na timu ya taifa, nitahakikisha kuwa niko tayari.” aliongeza Rooney.

Mchezaji wa Tottenham Eric Dier ataziba nafasi ya Rooney kwenye nafasi ya kiungo wakati timu yao itakapocheza na Slovenia.

Kocha wa Uingereza Southgate amesema kuwa “tumeangalia namna ambavyo Slovenia wanacheza na nikajua kabisa kwamba ni wachezaji wa aina gani nawahitaji kwenye sehemu ya kiungo. Kwahivyo maamuzi yangu hayana uhusiano wowote na kile kinachomtokea Wayne Rooney.”

Hata hivyo Wayne Rooney amesema kuwa kuachwa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa hakujambadilisha mawazo ya yeye kustaafu soka la kimataifa baada ya fainali za mwaka 2018 nchini Urusi.