KLABU BINGWA AFRIKA

Mamelodi Sundowns yatarajia kuweka historia michuano ya klabu bingwa Afrika

Wachezaji wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini wakishangilia wakati walipopata ushindi dhidi ya Zamalek
Wachezaji wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini wakishangilia wakati walipopata ushindi dhidi ya Zamalek STRINGER / AFP

Klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini inatarajia kuweka historia yake na kutumaini kuwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Zamalek iliyoupata juma moja lililopita ikiwa nyumbani, utatosha kuwafanya kuwa mabingwa wapya wa taji la klabu bingwa Afrika.

Matangazo ya kibiashara

Mamelodi itaingia uwanjani siku ya Jumapili ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Zamalek, huku historia ikionesha kuwa ni klabu ya Mouloudia Alger pekee miaka 40 iliyopita, ndio timu iliyofanikiwa kupindua matokeo ya mabao 3-0 na kutwaa taji hili.

Katika mchezo wa awali, Mamelodi ilicheza vizuri kiasi cha kutawala mchezo kwa muda wote wa mchezo, ambapo wadadisi wa masuala ya soka wanaona kuwa, huenda ikafanikiwa kuchomoza na ushindi mwingine mnono ugenini na kutwaa taji hilo.

Ikiwa Mamelodi inataka kujihakikishia nafasi ya kipekee ya kuweka historia kwa kutwaa taji hili, basi inahitaji angalau kupata bao la kuongoza kwenye dakika za awali za mchezo ili kuwavuruga wapinzani wao ambao bila shaka wataingia uwanjani wakiwa na nia ya kushambulia kutaka kurejesha mabao.

Hata hivyo kocha wa Mamelodi, Pitso Mosimane amelazimika kufanyia marekebisho safu yake ya ulinzi baada ya beki wake Wayne Arendse kuoneshwa kadi ya njano kwenye mchezo uliopita na hivyo kuukosa mchezo wa fainali.

Hii ina maana kuwa beki Thabo Nthethe atalazimika kucheza na Muivory Coast Bangaly Soum wachezaji ambao huwa hawachezo mara kwa mara pamoja na hivyo kuwa changamoto.

Hata hivyo kikosi chote cha Mamelodi kitasalia kama ilivyokuwa jijini Pretoria.

Zamalek yenyewe inajivunia kurejea kwa beki wake wa kushoto Ahmed Fathi ambaye hakuwa uwanjani kwa muda kutokana na kuwa majeruhi.

Kwenye mchezo wa awali kiungo wake mchambuliaji Maarouf Yusuf aliyekuwa amepewa jukumu la kucheza kama beki wa kushoto, huenda sasa akarejea kwenye nafasi yake kumpisha Fathi ambaye anarejea kwenye nafasi yake ya kushoto.