YANGA-TANZANIA

Sintofahamu yatanda kuhusu mustakabali wa klabu ya Yanga, baada ya kocha Pluijm kujiuzulu

Aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, ambaye sasa ametangaza kujiuzulu nafasi yake.
Aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, ambaye sasa ametangaza kujiuzulu nafasi yake. www.youngafricans.co.tz/

Kocha mkuu wa mabingwa wa soka nchini Tanzania, Yanga, Hans van der Pluijm, ametangaza kujiuzulu nafasi yake kwa kile mwenyewe alichosema ni sababu binafsi ambazo hawezi kuziweka wazi kwa uma.

Matangazo ya kibiashara

Kujiuzulu kwake kumekuja baada ya miezi kadhaa ya kuenea kwa uvumi kuwa uongozi wa klabu hiyo umepanga kumfuta kazi kocha huyo kutokana na matokeo mabaya ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata toka kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu ya soka bara.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa huenda kujiuzulu kwake kumetokana na taarifa za kuletwa kwa kocha mpya atakayekinoa kikosi hicho.

Kocha anayetajwa kuchukua nafasi ya Pluijm ni aliyekuwa kocha mkuu wa klabu ya Zesco United ya Zambia, George Lwandamina, ambaye anaelezwa kuwa yuko jijini Dar es Salaam kwa takribani juma moja sasa.

Kujiuzuli kwa Pluijm, kunaelezwa na wachambuzi wa soka kuwa ni kutokana na kocha huyo kuona ni jambo la heshima na busara kujiuzulu nafasi yake kabla ya kutangazwa kufutwa kazi yake, ambapo pia kulikuwa na taarifa huenda anegekuwa mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo, jambo ambalo yeye mwenyewe amekanusha.

Kocha Lwandamina, anatarajiwa kutangazwa rasmi juma lijalo kuwa kocha mkuu mpya wa Yanga, ambayo msimu huu wa mwaka 2016/2017, itashiriki kwa mara nyingine, michuano ya klabu bingwa barani Afrika.

Katika hatua nyingine, mabingwa hao wa soka nchini Tanzania, wamemteua Jerome Dufourg kuwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka 3, ambapo jukumu lake litakuwa ni kusimamia shughuli za klabu na hasa mfumo wake wa fedha.

Mfaransa Dufourg ameshawahi kufanya kazi na shirikisho la mpira wa miguu nchini Rwanda (Ferwafa) pamoja na klabu ya Talanta nchini Kenya, ambapo sasa amepewa jukumu la kubadili mfumo wa klabu hiyo.

Dufourg anatarajiwa kuanza kazi kwenye klabu hiyo kianzia November 19.

Katika mwaka mmoja uliopita mapato ya Yanga yalikuwa ni dola laki 5 sawa na bilioni 1.3 fedha ya Tanzania lakini matumizi yake yalikuwa ni zaidi ya dola milioni 1.3, ambapo mmiliki wa klabu hiyo na mwenyekiti wa klabu Yusuf Manji anasema ilijiendesha kwa hasara.