CC-TP MAZEMBE-BEJAIA

TP Mazembe katika harakati za kutengeneza historia nyingine kombe la shirikisho Afrika

Kikosi cha timu ya TP Mazembe ambacho kilicheza na Mo Bojaia ya Algeria.
Kikosi cha timu ya TP Mazembe ambacho kilicheza na Mo Bojaia ya Algeria. www.tpmazembe.com/en

Klabu ya TP Mazembe ya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, imejiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kutwaa taji la michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika, baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na klabu ya Mouloudia Bejaia ya nchini Algeria, katika mechi ya kwanza kati ya mbili za hatua ya fainali.

Matangazo ya kibiashara

Bao pekee la TP Mazembe lilifungwa na mchezaji Jonathan Bolingi, mchezaji pekee raia wa DRC kati ya wachezaji wanne wa DRC walioanza kwenye mchezo wa Jumamosi, October 29, goli alilofunga kwa njia ya Penati.

Nahodha wa klabu ya Bejaia, Faouzi Yaya aliisawazishia timu yake bao katika kipindi cha pili, akitumia mpira wa adhabu uliweka matumaini hai ya timu yake kubadili matokeo watakaposafiri kwenda nchini DRC.

Kocha mpya wa Algeria, Georges Leekens raia wa Ubelgiji, alikuwa miongoni mwa kelele za mashabiki takribani elfu 37 walioshuhudia mtanange huu ambao katika kipindi cha kwanza ulitawaliwa kwa sehemu kubwa na wanyeji, Bejaia.

Mo Bejaia ambayo inashiriki kwenye fainali za michuano hii kwa mara ya kwanza, italazimika kujilaumu kutokana na kupoteza nafasi nyingi kwenye kipindi cha kwanza, ambapo TP Mazembe walikuwa wanalinda goli lao muda mwingi.

Fainali ya pili ya kombe la shirikisho, itapigwa juma lijalo mjini Lubumbashi katika dimba la nyumbani la klabu ya TP Mazembe la Kamalondo, uwanja ambao umekuwa shubiri kwa timu nyingi ambazo zinasafiri kwenda DRC.