TP MAZEMBE-SOKA

TP Mazembe yajiweka kwenye nafasi nzuri

Baadhi ya wachezaji wa TP Mazembe ya DRC wakishangilia moja ya magoli ambayo timu yao ilifunga.
Baadhi ya wachezaji wa TP Mazembe ya DRC wakishangilia moja ya magoli ambayo timu yao ilifunga. goal.com

Klabu ya soka ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imejiweka katika nafasi nzuri ya kushinda taji la Shirikisho barani Afrika, baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 katika fainali ya kwanza dhidi ya MO Bejaia ya Algeria mwishoni mwa wiki iliyopita.

Matangazo ya kibiashara

Jonathan Bolingi aliifungia Mazembe bao hilo muhimu kupitia mkwaju wa penalti katika kipindi cha kwanza katika mchuano uliochezwa mjini Blida.

Nahodha wa MO Bejaia, Faouzi Yaya, aliisawazishia klabu yake baada ya kucheza mkwaju wa nidhamu uliojaa wavuni katika kipindi cha pili.

Mchuano wa marudiano utachezwa siku ya Jumapili mjini Lubumbashi, mechi ambayo Mazembe wanatarajiwa kupata ushindi ili kunyakua taji hili baada ya kumaliza katika nafasi ya pili miaka mitatu iliyopita.

TP Mazembe inakwenda kwenye mchuano huu ikiwa na historia ya kuwahi pia kushinda mataji matano ya klabu bingwa barani Afrika.

Mshindi wa taji hili atapokea Dola za Marekani 660,000 huku atakayeibuka wa pili akipata Dola za Marekani 462,000 lakini pia atacheza fainali ya Super Cup dhidi ya Sundowns ya Afrika Kusini iliyoshinda taji la klabu bingwa barani Afrika msimu huu.