TENESI

Konta aanza vema mashindano ya Elite nchini China

Muingereza, Johanna Konta.
Muingereza, Johanna Konta. Reuterss/Issei Kato

Mchezaji tenesi namba moja kwa nchi ya Uingereza kwa wanawake Johanna Konta, ameanza vema mashindano ya Elite, baada ya kumfunga Muaustralia Sam Stosur kwa seti mbili bila kwa matokeo ya 6-4 na 6-2, jijini Zhuhai, China.

Matangazo ya kibiashara

Mashindano haya yanahusisha wachezaji 12 wanaoongoza kwa mchezo wa tenesi duniani, ambao hawakufanikiwa kufuzu kwenye mashindani ya juma lililopita ya fainali ya WTA nchini Singapore.

Wachezaji wamegawanywa kwenye makundi manne ya wachezaji watatu watatu, huku mshindi katika kila kundi anafuzu katika hatua ya mtoano.

Konta ambaye anatarajiwa kung'ara kwenye mashindano haya, atakutana na mchezaji namba 23 kwenye orodha ya ubora wa mchezo huo, Caroline Garcia wa Ufaransa, katika mechi yake ingine.

Muingereza Konta alionekana toka awali kumzidi kwa kila kitum bingwa wa michuano ya US Open wa mwaka 2011, Sam Stosur, ambapo alimshinda kirahisi katika seti ya kwanza tu ya mchezo.

Konta mwenye umri wa miaka 25 hivi sasa, amejihakikishia nafasi ya kumaliza kwenye nafasi ya 10 bora ya orodha ya wanawake, ambapo atakuwa mchezaji wa kwanza Muingereza upande wa wanawake kufanya hivyo toka alipofanya hivyo, Muingereza mwingine, Jo Durie mwaka 1983.