DRC. TP MAZEMBE-MO BEJAIA

TP mazembe na MO Bejaia kumenyana Jumapili mjini Lubumbashi

TP Mazembe wakati wa michuano ya Kombe la Dunia ya klabu 2015.
TP Mazembe wakati wa michuano ya Kombe la Dunia ya klabu 2015. KAZUHIRO NOGI / AFP

Shirikisho la soka barani Afrika CAF, limewateua marefarii kutoka nchini Senegal kuchezesha mchuano wa pili wa fainali kati ya TP Mazembe ya DRC na MO Bejaia ya Algeria, kuwania taji la Shirikisho barani Afrika.

Matangazo ya kibiashara

Mchuano huu utachezwa siku ya Jumapili mjini Lubumbashi.

Marefarii hao watatu ni pamoja na Malang Diedhiou atakayekuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na wenzake Djibril Camara na El Hadji Malick Samba.

Diedhiou mwenye umri wa miaka 43, ana uzoefu mkubwa kama mwamuzi baada ya kuanza kuchezesha mechi za kimataifa mwaka 2008.

Mwaka huu wakati wa michezo ya Olimpiki nchini Brazil, mwamuzi huyu alichezesha mchuano dhidi ya Fiji na Korea na Japan dhidi ya Sweden.

Fainali hii inakuja baada ya mchuano wa kwanza mwishoni wa wiki iliyopita kumalizika kwa sare ya bao 1-1 ugenini.
TP Mazembe inakwenda kwenye mchuano huu ikiwa na historia ya kuwahi pia kushinda mataji matano ya klabu bingwa barani Afrika.

Mshindi wa taji hili atapokea Dola za Marekani 660,000 huku atakayeibuka wa pili akipata Dola za Marekani 462,000 lakini pia atacheza fainali ya Super Cup dhidi ya Sundowns ya Afrika Kusini iliyoshinda taji la klabu bingwa barani Afrika msimu huu.