CAF-SOKA

TP Mazembe wanyakua taji la Shirikisho barani Afrika

Wachezaji wa TP Mazembe Christian Kouamé Koffi , Adama Traoré na  Jonathan Bolingi wakisherehekea baada ya kuifunga Mo Bejaia fainali ya taji la Shirikisho barani Afrika.
Wachezaji wa TP Mazembe Christian Kouamé Koffi , Adama Traoré na Jonathan Bolingi wakisherehekea baada ya kuifunga Mo Bejaia fainali ya taji la Shirikisho barani Afrika. stringer / AFP

Klabu ya soka ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ndio mabigwa wapya wa taji la Shirikisho barani Afrika mwaka 2016, baada ya kuishinda Mo Bejaia ya Algeria mabao 4-1 katika fainali ya pili iliyochezwa Jumapili jioni katika uwanja wa Kamalondo mjini Lubumbashi.

Matangazo ya kibiashara

Kwa ujumla, Mazembe walipata ushindi wa mabao 5-2 kwa sababu fainali ya  kwanza, walitoka sare bao 1-1 wiki moja iliyopita, walipocheza ugenini.

Rainford Kalaba mchezaji wa Kimataifa kutoka Zambia katika mchuano huo, aliifungia timu yake mabao 2, na kuibuka mfungaji bora katika mashindano haya kwa kuifungia Mazembe kwa jumla ya mabao 8.

Hili ni taji la kwanza la TP Mazembe, baada ya mwaka 2013 kumaliza katika nafasi ya pili katika michuano hii.

Pamoja na taji hili, Mazembe imepata Dola za Marekani 660,000 huku Mo Bejaia ikijinyakulia Dola za Marekani 462,000 kutoka kwa Shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Mabingwa hawa wapya watacheza fainali ya Super Cup dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyoshinda taji la klabu bingwa barani Afrika msimu huu. Mechi hiyo itachezwa mapema mwaka 2017.

Vlabu vingine ambavyo vimewahi kunyakua taji hili ni pamoja na CS Sfaxien ya Tunisia ambayo inashikilia rekodi ya kushinda mara tatu mwaka 2007, 2008 na 2013 ikifuatwa na Etoile du Sahel pia kutoka Tunisia ikiwa imeshinda mara mbili mwaka 2006 na 2015.