FIFA-SOKA

Qatar yasema uamuzi wa kuandaa kombe la dunia mwaka 2022 hauwezi kubadilishwa

Nembo la kombe la dunia nchini Qatar 2022
Nembo la kombe la dunia nchini Qatar 2022

Kamati andalizi ya michuano ya soka kuwania kombe la dunia itakayofanyika nchini Qatar mwaka 2022, inasema uamuzi wa nchi hiyo kuwa wenyeji wa michuano hiyo mikubwa duniani haiwezi kubadilishwa.

Matangazo ya kibiashara

Tangazo hili limetolewa siku ya Jumatatu licha ya kuwepo kwa madai ya ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wafanyikazi wakati huu Qatar ikikarabati viwanja mbalimbali.

“Kombe la dunia mwaka 2022 litafanyika Qatar na kwa mara ya kwanza katika eneo la Mashariki ya Kati. Hakuna mabadiliko yatakayofanyika kuhusu hilo,” amesema Hassan al-Thawadi Katibu Mkuu wa Kamati hiyo andalizi.

Ofisi ya mwanasheria Mkuu nchini Uswizi inachunguza madai ya kuwepo kwa madai ya ufisadi kuwa Qatar ilitoa rushwa ili kupigiwa kura kushinda uwenyeji wa kombe la dunia.

Qatar imekuwa ikijenga viwanja vipya ili kufikia idadi inayohitajika ya viwanja 12 lakini imeendelea kukabiliana na kukeuka haki za wafanyikazi wanaojenga viwanja hivyo, madai ambayo nchi hiyo inakanusha.

Serikali ya Qatar inasema itatumia zaidi ya Dola Bilioni 10 kujenga viwanja vitakavyotumiwa katika mashindano hayo.

Baada ya kombe ka dunia mwaka 1978 nchini Argetina, viwanja 12 vimekuwa vikitumiwa kuandaa michuano hiyo na inavyoonekana, huenda viwanja nane ndivyo vitakuwa tayari kufikia mwaka huo.