SOKA

Serikali ya Sudan Kusini yalaani kuuawa kwa mashabiki wa soka jijini Juba

Eneo walikopigwa risasi mashabiki wa soka mjini Juba Novemba 6 2016
Eneo walikopigwa risasi mashabiki wa soka mjini Juba Novemba 6 2016 static.pulse.com.

Serikali ya Sudan Kusini imelaani mauaji ya mashabiki nane waliopigwa risasi na kuuawa mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati wakitazama mchuano wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza jijini Juba.

Matangazo ya kibiashara

Naibu Waziri wa Habari nchini humo Paul Akol Kordit amesema watu wasiojulikana walivamia baa hiyo na kuwafwatulia risasi mashabiki hao na kuwajeruhi wengine wakati wakishabikia timu zao.

Serikali ya Juba inasema itawachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuhusika na mauaji haya lakini pia imetoa hakikisho kwa mashabiki wa soka nchini humo kuwa itawalinda.

Suala la ukosefu wa usalama limekuwa likishuhudiwa jijini Juba kwa miaka mitatu sasa na hali imekuwa mbaya mwaka huu, hali ambayo imeendelea kuzua hali ya wasiwasi katika mji huo mkuu.