Katibu Mkuu wa FIFA kuzuru Sierra Leone
Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka duniani FIFA Fatma Samoura anatarajiwa kuzuruĀ Sierra Leone kusaidia kutatua mzozo ka Shirikisho la soka nchini humo na serikali.
Imechapishwa:
Bi.Samoura ameomba kukutana na rais wa nchi hiyo Ernest Bai Koroma na viongozi wengine kujaribu kupata suluhu.
Ziara hiyo inatarajiwa kufanyika tarehe 16 mwezi huu na Katibu Mkuu huyo amesema ana imani kuwa mwafaka utapatikana baada ya mazungumzo hayo.
Kumekuwa na madai ya Sierra Leone kuhusika na upangaji wa matokeo hasa mwaka 2008 wakati nchi hiyo ilipomenyana na Afrika Kusini na kulazimisha sare ya kutofungana katika mchuano muhimu wa kufuzu kucheza fainali ya mataifa bingwa.
Mwaka 2014, wachezaji 15 wa timu ya taifa walisimamishwa kuendelea kucheza soka nchini humo baada ya kushukiwa kuhusika.
Kashfa hii imesababisha serikali kuingilia kati ripoti ya uchunguzi wa Shirikisho la soka nchini humo kuhusu madai hayo ambayo ipo mikononi mwa serikali ambayo haijatolewa wazi.
Serikali ya Siere Leon pia imekuwa ikimshtumu rais wa Shirikisho la soka nchini humo Isha Johansen, kuhusika na ufisadi na hata aliwahi kukamatwa na kuhojiwa na tume ya kupambana na ufisadi kuhusu madai ya kupotea kwa fedha za Shirikisho hilo.
Kanuni za FIFA haziruhusu serikali kuingilia maswala ya soka na nchi wanachama inapokeuka hali hii huwa inafungiwa na FIFA.